Njoo, Unifuate
Oktoba 12–18. “Mkombozi Atakuja Sayuni”: Isaya 58–66


Oktoba 12–18. ‘Mkombozi Atakuja Sayuni’: Isaya 58–66” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani: Agano la Kale 2026 (2026)

Oktoba 12–18. ‘Mkombozi Atakuja Sayuni,’” Njoo, Unifuate: Agano la Kale 2026

Yesu akisoma hati ya kukunja kwa watu katika sinagogi

Yesu katika Sinagogi huko Nazareti, na Greg Olsen

Oktoba 12–18: “Mkombozi Atakuja Sayuni”

Isaya 58–66

Mwanzoni mwa huduma yake ya duniani, Yesu Kristo alitembelea sinagogi huko Nazareti, kijiji ambacho Yeye alilelewa. Yeye alisimama kusoma kutoka kwenye maandiko, akafungua kitabu cha Isaya, na kusoma kile tunachojua sasa kama Isaya 61:1–2. Kisha Yeye akatangaza, “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.” Hii ilikuwa mojawapo ya matamko ya moja kwa moja ya Mwokozi kwamba Yeye ndiye Mpakwa Mafuta, ambaye “atawaponya waliovunjika moyo” na “kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao” (ona Luka 4:16–21). Maandiko haya kwa kweli yalitimia siku hiyo. Na, kama vile unabii mwingi wa Isaya, unaendelea kutimia katika siku zetu. Mwokozi anaendelea kuwaponya waliovunjika moyo ambao huja Kwake. Bado kuna mateka wengi ambao wanahitaji ukombozi. Na kuna mazuri ya baadaye ya kujiandaa kwa ajili yake—wakati ambapo Bwana “ataumba mbingu mpya na dunia mpya” (Isaya 65:17) na “kuotesha haki na sifa mbele ya mataifa yote” (Isaya 61:11). Kusoma Isaya kunatufungua macho yetu kwa kile Bwana amekwisha kifanya, kile anachofanya, na kile atakachowafanyia watu Wake.

ikoni ya kujifunza

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Isaya 58:3–12

ikoni ya seminari
Kufunga hujenga nguvu za kiroho na hubariki watu walio katika shida.

Kwa nini mtu yeyote kwa hiari huacha kula chakula wakati chakula kinapatikana? Unapojifunza Isaya 58:3–12, unaweza kufikiria kuhusu sababu zako za kufunga—vile vile sababu za Bwana za kutoa sheria hii. Haya ni baadhi ya maswali ya kutafakari:

  • Kwa nini kufunga wakati mwingine kunaweza kuonekana kama mzigo zaidi kuliko baraka? ( ona Isaya 58:3–5). Ni kwa jinsi gani mafundisho ya Bwana katika sura hii yanabadilisha mtazamo huo kwako?

  • Inaweza kumaanisha nini “kufungua kamba za uovu” na “kuvunja kila nira”? (Isaya 58:6). Ni kwa jinsi gani kufunga kunaweza kuwabariki wengine? (ona mstari wa 7).

  • Ni kwa namna gani kufunga kumekuletea baraka zilizoelezwa katika Isaya 58:8–12?

Katika ujumbe wake, “Je, Saumu Niliyoichagua, Siyo ya Namna Hii?” (Liahona, Mei 2015, 22–25), Rais Henry B. Eyring alishiriki mifano kadhaa ya jinsi watu walivyobarikiwa kwa kufunga na matoleo ya mfungo. Ni kwa jinsi gani umeshuhudia baraka kama hizo katika maisha yako?

Ona pia “Bless Our Fast, We Pray,” Nyimbo za Dini, na. 138; Mada na Maswali, “Kufunga na Matoleo ya Mfungo,” Maktaba ya Injili.

Pata kuwajua watu unao wafundisha. “Kuwa mwalimu kama Kristo kunajumuisha kuwajua watu unao wafundisha na kujitahidi kuelewa kile kilichoko mioyoni mwao. … Unaweza kuona jinsi wanavyojifunza vizuri zaidi. Unaweza kuuliza maswali, kusikiliza kwa makini, na kutazama. Zaidi ya yote, unaweza kusali ili upate uelewa ambao Roho pekee ndiye anayeweza kutoa. Kadiri unavyomwelewa vyema mtu, ndivyo unavyoweza vyema kumsaidia kupata maana binafsi na nguvu katika injili ya Yesu Kristo. Mara unapokuwa umeelewa kiu ya mtu, Roho anaweza kukufundisha jinsi ya kusaidia kuzima kiu hiyo kwa maji ya uzima ya Mwokozi” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi13).

Isaya 58:13–14

Kumheshimu Bwana siku ya Sabato kunaleta shangwe.

Je, siku ya Sabato ni “ya kupendeza” kwako? Unapojifunza Isaya 58:13–14, fikiria jinsi ambavyo ungeweza kupata furaha zaidi katika siku za Bwana. Kwa mfano, inaweza kumaanisha nini kugeuka “usifanye anasa yako kwenye siku [Yake] takatifu”? Kuna tofauti gani kati ya “[kujifurahisha] mwenyewe katika Bwana” na “kufanya njia zako mwenyewe”?

Ona pia Russell M. Nelson, “Sabato ni Furaha,” Liahona,” May 2015, 129–32.

Isaya 59:9–21; 61: 1– 3; 63:7–9

Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wangu.

Isaya 58–66 ina marejeleo mengi juu ya misheni ya upatanisho wa Yesu Kristo. Yatafute wakati unapojisomea. Hasa, tilia maanani majina na maneno yaliyotumika kumwelezea Mwokozi. Kwa mfano:

  • Ni nini kinachokuvutia kuhusu maelezo ya “mwombezi” katika Isaya 59:16–21? Ni kwa jinsi gani Mwokozi anashinda hali zilizoelezewa katika mstari wa 9–15?

  • Wakati Yesu Kristo alipotangaza kwa watu wa Nazareti kwamba Yeye alikuwa Masiya, Yeye alinukuu kutoka katika Isaya 61:1–3 (ona Luka 4:16–21; ona pia video “Jesus Declares He Is the Messiah,” Maktaba ya Injili). Je, ni kwa jinsi gani Yesu Kristo amekubariki wewe na wengine katika njia zilizoelezewa katika mistari hii? Je! Ni kwa jinsi gani Yeye ametoa uzuri badala ya majivu?

    3:24

    Jesus Declares He Is the Messiah

  • Ni “fadhili za Bwana” gani unaweza “kutaja”? ( ona Isaya 63:7–9).

  • Je, unapata marejeo gani mengine kwa Mwokozi katika Isaya 58–66?

Ona pia Mosia 3:7; Mafundisho na Maagano 133:46–53.

mikono ya mwanaume akimfikia kwa taa ya mafuta ili kuwasha taa ya mwanamke

Zawadi ya Nuru, na Eva Timothy

Isaya 60; 62

“Bwana atakuwa nuru ya milele kwako.”

Isaya 60 na 62 zinazungumza juu ya nuru na kiza, macho na kuona ili kufundisha jinsi gani injili ya Yesu Kristo itakavyo ubariki ulimwengu katika siku za mwisho. Tafuta dhana hizi hususani katika Isaya 60:1–5, 19–20; 62:1–2. Unaposoma sura hizi, tafakari jinsi Mungu anavyowakusanya watoto Wake toka gizani kuja kwenye nuru Yake. Jukumu lako ni lipi katika kazi hii?

Ona pia 1 Nefi 22:3–12; 3 Nefi 18:24; Mafundisho na Maagano 14:9; Bonnie H. Cordon, “Ili Wapate Kuona,” Liahona, Mei 2020, 78–80.

Isaya 64:1–5; 65:17–2566

Kristo atatawala duniani wakati wa Milenia.

Isaya alisema juu ya siku ambapo “taabu za kwanza zimesahauliwa” (Isaya 65:16). Wakati unabii huu una utimilifu kadhaa, kwa maana yake kamili, siku hiyo bado haijafika—wakati Yesu Kristo atakaporudi. Isaya anaielezea siku hii ya baadaye katika Isaya 64:1–5; 65:17–2566. Angalia ni mara ngapi alitumia maneno kama “furahi” na “kufurahia.” Kwa nini kurudi kwa Mwokozi itakuwa siku ya furaha kwako? Je, unaweza kufanya nini kujiandaa kwa ajili ya ujio Wake?

Ona pia Makala ya Imani 1:10; Russell M. Nelson, “Siku za Baadaye za Kanisa: Kuuandaa Ulimwengu kwa Ajili ya Ujio wa Pili wa Mwokozi,” Liahona, Apr. 2020, 13.

Kwa ajili ya zaidi, ona matoleo ya mwezi huu ya majarida ya Liahona na Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana. .

ikoni ya sehemu ya watoto

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Isaya 58:6–11

Kufunga kunanibariki mimi na wengine wenye mahitaji.

  • Pengine njia bora zaidi ya kuwahimiza watoto wako wafunge—wanapokuwa tayari—ni kuwasaidia kuelewa madhumuni ya Bwana kwa ajili ya sheria hii. Fikiria kusoma pamoja Isaya 58:6–11 ili kupata majibu ya maswali haya: Kwa nini sisi tunafunga? Tunafunga kwa namna gani? Ungeweza pia kuangalia katika “Mfungo, Kufunga” katika Mwongozo wa Maandiko.

  • Kama umekuwa na uzoefu wa maana wa kufunga, ushiriki na watoto wako. Ungeweza pia kuwauliza jinsi ambavyo wangemwelezea rafiki kwa nini Bwana alitupatia sheria hii.

Isaya 58:13–14

Sabato inaweza kuwa ya furaha kwangu.

  • Baada ya kusoma Isaya 58:13–14, ungeweza kuonyesha siku za wiki kwenye kalenda na waalike watoto wako waseme siku pamoja nawe. Unapofika Sabato, waombe waite siku hiyo “furaha.” Waambie wao kwa nini Sabato ni ya furaha kwako.

  • Shirikianeni njia mnazoweza “kujifurahisha mwenyewe katika Bwana” siku ya Sabato. Pengine watoto wako wangeweza kuchora mawazo yao na kuyaweka katika “sanduku la furaha ya Sabato.” Kisha, wanapohitaji mawazo kuhusu mambo ya kufanya siku ya Sabato, wangeweza kuvuta wazo kutoka kwenye sanduku.

picha ya Yesu

Nuru Yetu, na Dan Wilson

Isaya 60:1–3

Mwokozi ni kama nuru kwangu.

  • Waalike watoto wako wafumbe macho yao wakati unaposoma Isaya 60:1–3. Waombe wafumbue macho yao pale wanaposikia neno “nuru” na kuyafumba pale wanaposikia neno “giza.” Eleza kwamba Yesu Kristo na injili Yake ni kama nuru inayotusaidia kuona njia yetu ya kurudi kwa Baba wa Mbinguni.

Isaya 65:17–25

Yesu atakapokuja tena, Yeye ataleta amani na shangwe.

  • Isaya 65:17–25 inafafanua vile dunia itakavyokuwa wakati Mwokozi atakapokuja tena. Unaposoma mistari hii pamoja na watoto wako, wasaidie watafute jinsi maisha yatakavyokuwa tofauti katika “dunia mpya” Isaya aliyoelezea. Kwa nini huu utakuwa wakati wa “kufurahi na kushangilia daima”? (mstari wa 18).

  • Mngeweza pia kuimba pamoja wimbo kuhusu Ujio wa Pili, kama vile “When He Comes Again” (Gospel Library). Shirikiane ninyi kwa ninyi kile mnachotazamia kuhusu kurudi kwa Mwokozi. Je, tunaweza kufanya nini ili kujiandaa kwa ajili ya siku hiyo?

Kwa ziada, ona toleo la mwezi huu la jarida la Rafiki.

Yesu Kristo angani, akiitoa nuru

“Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzuguka.” (Isaya 60:1). Nuru na Uzima, na Mark Mabry

Ukurasa wa shughuli ya Watoto: Sabato inaweza kuwa ya furaha kwangu