2025
Maagano, Nguvu, na Ahadi
Oktoba 2025 Liahona


"Maagano, Nguvu, na Ahadi," Liahona, Okt. 2025.

Ujumbe wa kila Mwezi wa Liahona, Oktoba 2025

Maagano, Nguvu, na Ahadi

Hekalu ni kitovu cha nguvu na ulinzi ulioahidiwa kwa waaminifu kabla ya Ujio wa Pili wa Bwana Yesu Kristo.

kielelezo cha Joseph Smith akiwa amesimama mbele ya Hekalu la Kirtland

Kielelezo cha Joseph Smith na Dan Burr

Mnamo Mei 1833, babu yangu mkuu wa nne Asahel Perry na baadhi ya marafiki walisafiri kutoka kaskazini mwa New York hadi Kirtland, Ohio. Hawakuwa waumini wa Kanisa jipya lililorejeshwa, lakini walitaka kukutana na Nabii Joseph Smith. Walifika katika muda muafaka wa kuhudhuria baraza la kwanza lililofanyika ili kujadili ujenzi wa Hekalu la Kirtland.

Baada ya mkutano wa baraza kuanza, Nabii aliwasilisha shughuli kuhusu ujenzi hekalu. Kisha akawaomba wale waliokuwepo kuelezea hisia zao zinazohusiana na kazi kubwa kama hiyo. Wengi walijibu kwamba Kanisa lilikuwa duni sana kukabiliana na kazi kama hiyo. Walipendekeza ujenzi wa jengo dogo, lisilo na gharama kubwa.

Wakati wa majadiliano yaliyofuatia, Babu Perry na rafiki zake walikusanya, wakatoa pesa zao, na kuongeza. Je, walikuwa na za kutosha kulipia safari yao ya kurudi na kuchangia kwenye ujenzi wa hekalu? Dakika chache baadaye, babu yangu alimwendea Joseph Smith, alitoa sarafu ya dhahabu ya dola tano, na kuiwasilisha kwa Nabii. (Sarafu kama hiyo leo itakuwa na thamani ya mamia ya dola!)

Joseph alisimama mbele ya baraza na kuinua juu sarafu hiyo. Kisha, akizungumza kwa ujasiri, alisema kwamba "kazi ilikuwa imeanza na Nyumba [ya Bwana] ingejengwa kulingana na mpangilio uliowasilishwa" na Bwana Yesu Kristo.

Familia ya Perry punde ilijiunga na Kanisa huko Kirtland, ilipokea baraka zao za hekaluni miaka michache baadaye katika Hekalu la Nauvoo, na baadaye kuvuka nyanda kwenda Utah.

Wakati Hekalu la Kirtland lilipowekwa wakfu mwaka 1836, lilikuwa dogo mno kuenea Watakatifu wa Siku za Mwisho wote waliotaka kuhudhuria kuwekwa wakfu kwake. Kadiri Kanisa lilivyotanuka, ndivyo idadi ya Watakatifu waliolazimika kuhudhuria mikutano nje. Rais James E. Faust (1920–2007), ambaye alihudumu kama rais wangu wa kigingi nilipokuwa kijana na kama mnasihi wakati nilipoitwa kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka mwaka 2007, alitoa maoni haya kuhusu hekalu la pili la Kanisa:

"Kabla ya Hekalu la Nauvoo kukamilika mnamo 1846 Watakatifu wangekutana nje, mara nyingi karibu na hekalu, kumsikiliza Joseph na viongozi wengine wa Kanisa wakizungumza. Wakati mwingine maelfu walihudhuria mikutano hiyo"—wakati mwingine hata katika hali mbaya ya hewa.

"Kama [Mzee] George A. Smith alivyoelezea katika njia yake ya ucheshi, ’Katika siku za Nabii Joseph … [Kanisa] lilistawi vizuri zaidi kwa watu kukutana nje.’"

Tunashukuru kwamba katika siku zetu, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linastawi nje, ndani, na kote ulimwenguni. Kustawi huko kunajumuisha ujenzi wa mahekalu kwa kasi isiyo na kifani "kulingana na mpangilio uliowasilishwa"—mpangilio ambao daima umejumuisha baraka, kujitolea, imani, na dhabihu.

Kielelezo cha Hekalu la Kirtland

Nuru Tukufu—Hekalu la Kirtland, na Glen S. Hopkinson, isinakiliwe

Kwa Nini Mahekalu Mengi Sana?

"Watangulizi wetu walitoa unabii kwamba mahekalu yatajaa Amerika ya Kaskazini na Kusini, visiwa vya Pasifiki, Ulaya, na kwingineko," Rais Eza Taft Benson (1899–1994) alisema miongo kadhaa iliyopita. "Kama kazi hii ya ukombozi itafanyika kwa kiwango ambacho lazima ifanyike, mamia ya mahekalu yatahitajika."

Rais Russell M. Nelson alisema tunajenga mahekalu kwa kasi isiyo na kifani leo "kwa sababu Bwana ametuamuru tufanye hivyo. Baraka za hekalu husaidia kukusanya Israeli pande zote mbili za pazia. Baraka hizi pia zinasaidia kuwaandaa watu ambao watasaidia kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana!"

Katika sala yake ya kuweka wakfu Hekalu la Kirtland, Joseph Smith aliomba "kwamba watu wote watakaoingia kwenye lango la nyumba ya Bwana na waweze kuhisi nguvu zako. …

"Na tunakuomba wewe, Baba Mtakatifu, kwamba watumishi wako wapate kwenda katika nyumba hii wakiwa wamevikwa uwezo wako, na kwamba jina lako liweze kuwa juu yao, na utukufu wako uwazingire pande zote, na malaika zako wawalinde" (Mafundisho na Maagano 109:13, 22 ; msisitizo umeongezwa; ona pia mstari wa 23).

Ninaposoma mistari hiyo, ninatafakari juu ya ono la Nefi la siku za mwisho. Zingatia maneno sawa na hayo: "Na ikawa kwamba mimi, Nefi, niliona nguvu za Mwanakondoo wa Mungu, kwamba ziliwashukia watakatifu wa kanisa la Mwanakondoo, na kwa watu wa agano wa Bwana, ambao walitawanyika kote usoni mwa dunia; na walikuwa wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu (1 Nefi 14:14; msisitizo umeongezwa).

Ninaamini kwamba mahekalu ya siku za mwisho yana nafasi muhimu katika kutimiza unabii wa Nefi na ni kitovu cha ulinzi na nguvu zilizoahidiwa kwa waaminifu kabla ya Ujio wa Pili.

Miaka kadhaa iliyopita, wakati nikihudumu kama askofu wa kata ya chuo kikuu, nilishangazwa hususani na msichana mmoja katika kata yangu. Bado ananishangaza. Mnamfahamu kama Rais Emily Belle Freeman, Rais Mkuu wa Wasichana. Katika hotuba ya mkutano mkuu wa hivi karibuni, alifundisha kwamba kupitia hekalu, Yesu Kristo hutuinua hadi kwenye usawa wa juu wa kiroho.

"Kila wakati ninapovuka lango la nyumba Yake, ninapata uhusiano wa kina wa agano na Yeye," Rais Freeman alisema. "Mimi nilitakaswa na Roho Wake, nilipata endaumenti kwa nguvu Zake, na kusimikwa kuujenga ufalme Wake."

Nguvu Iliyoahidiwa

Rais Nelson amezungumza mara nyingi kuhusu nguvu ya Yesu Kristo inayopatikana kupitia maagano ya hekaluni. "Kujifunga mwenyewe nira na Mwokozi inamaanisha unaweza kufikia nguvu Zake na uwezo wa kukomboa," alisema. Rais Nelson pia amefundisha:

"Tunaposhika maagano yetu ya hekaluni, tunapata fursa kubwa zaidi ya nguvu za kuimarisha za Bwana. Ndani ya hekalu, tunapokea ulinzi dhidi ya mapigo ya ulimwengu."

"Ibada muhimu za [Mwokozi] zinatuunganisha Kwake kupitia maagano matakatifu ya ukuhani. Kisha, tunaposhika maagano yetu, Yeye hututunuku na nguvu Zake za uponyaji, za kuimarisha. Na ee, jinsi gani tutakavyohitaji nguvu Zake katika siku zijazo."

"Nguvu ya kimaadili na ya kiroho ambayo watu wetu wanaihitaji hivi sasa na kwa siku zijazo ni nguvu ya Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo. Tunapata kuifikia nguvu Yao kwa kufanya na kushika maagano tuliyoweka Nao."

Nguvu za mbinguni ni muhimu, akina kaka na akina dada, kwa sababu tunaishi katika ulimwengu wenye uovu sana. Bila nguvu hiyo, hatutaweza "kustahimili siku ya kuja kwake" au "kusimama atakapokuja" (Malaki 3:2). Hatujui ni lini siku hiyo itakuwa, lakini mjumbe Wake tayari ametumwa "kuitengeneza njia" kwa ajili ya ujio Wake (Malaki 3:1). Wakati huo huo, ulimwengu hausongi kwa utulivu kuelekea siku hiyo.

Tunahitaji nguvu iliyoahidiwa kwa waaminifu ili kutusaidia:

  • Kuacha Mungu ashinde katika maisha yetu.

  • Kutubu na kusogea karibu zaidi na Bwana.

  • Kubariki, kufariji, kuongoza, na kuhudumia.

  • "Kustahimili vizuri zaidi majaribio yetu, majaribu, na huzuni kubwa" (onaMosia 3:19.

  • Kupata amani na shangwe katika Kristo tunapotembea kwenye njia ya agano.

  • Kujiandaa "dhidi ya siku ya mchomo" na "majanga ya waovu" (Mafundisho na Maagano 109:46).

  • Kukamilisha kazi ya Bwana kabla ya Ujio Wake wa Pili.

Hekalu la Tucson Arizona

Picha ya sehemu ya juu ya Hekalu la Tucson Arizona na James Whitney Young

Walinzi wa Wokovu

Kazi na utukufu wa Baba wa Mbinguni ni "kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu" (Musa 1:39). Kila hekalu linasimama kama mlinzi wa kidunia wa mpango wa Mungu wa wokovu, likielekezea kwenye jukumu kuu la Mwokozi katika kazi hiyo na utukufu.

Akiwa amejihami kwa nguvu Zake, kila mwanaume na mwanamke anayeshika maagano—aliyeoa/kuolewa au la—ambaye kwa uaminifu hushika maagano ya hekaluni atabarikiwa katika maisha haya na katika maisha yajayo.

Rais Nelson ameahidi: "Hatma ambayo kila mmoja wetu anajitahidi kuipata ni ile ya kupata endaumenti ya nguvu katika nyumba ya Bwana, kuunganishwa kama familia, uaminifu kwenye maagano yaliyofanywa katika hekalu ambayo yanatustahilisha kwa ajili ya zawadi kuu ya Mungu—ile ya uzima wa milele. Ibada za hekaluni na maagano unayofanya huko ni muhimu katika kuimarisha maisha yako, ndoa yako na familia yako, na uwezo wako wa kukinzana na mashambulizi ya adui. Kuabudu kwako hekaluni na huduma yako huko kwa ajili ya mababu zako kutakubariki na ongezeko la ufunuo binafsi na amani na kutaimarisha nia yako ya kubaki kwenye njia ya agano."

Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninashuhudia kwamba vitu hivi ni vya kweli.