"Ushindi wa Mwokozi Wetu Mpendwa," Liahona, Apr. 2026.
Ujumbe wa kila Mwezi wa Liahona, Aprili 2026
Ushindi wa Mwokozi Wetu Mpendwa
Hakuna maneno ya kuelezea ukubwa wa zawadi ya thamani ya Yesu Kristo. Kamwe haitahitajika kutoka kwa mwingine. Yeye aliteseka "mara moja tu."
Kadiri miaka ambavyo imepita, nimezidi kunyenyekezwa kadiri nilivyofikiria kuhusu, kujifunza, na kupata faraja kubwa katika zawadi isiyopimika ya Mwokozi wetu, Upatanisho wa Yesu Kristo. Akili za binadamu haziwezi kuanza kuelewa jinsi hatima ya wanadamu ilivyobadilika kabisa kwa sababu ya kile kilichotokea Gethsemane, msalabani, na kaburini.
Sote Tunakumbana na Kuvunjika Moyo na Mateso
Katika wito wangu kama Mtume, nimesafiri sana na nilikuwa na fursa ya kukutana na watoto, vijana, na watu wazima kote ulimwenguni. Kuna nyakati za shangwe kuu katika maisha, lakini kitu kimoja ambacho nimekiona kwa macho yangu mwenyewe na kuhisi kwa kina moyoni mwangu ni kwamba pamoja na furaha na shangwe, maisha huwa na nyakati za kuvunjika moyo na mateso.
Siwezi kamwe kusahau nikikaa pamoja na watoto wanne wadogo ambao maisha ya wazazi wao yalitamatishwa kikatili na mvamizi katika nyumba yao wenyewe wakati watoto wakiwa wamelala, au kukutana na mwanamke ambaye alikuwa amenyanyaswa kama msichana na ndugu wa kuaminika, au kukaa kando ya kitanda cha msichana mdogo ambaye alipata jeraha kwenye ubongo baada ya kuanguka kutoka kwenye baiskeli na ambaye punde angefariki, au kusikiliza kilio cha mwanamke ambaye mume wake alikuwa amemsaliti yeye pamoja na maagano ya hekaluni katika njia mbaya isiyoelezeka kwa miaka mingi.
Nimehisi maumivu ya wenza ambao mtoto wao mkubwa hakuamini tena kweli za injili na akitafuta kudhoofisha imani ya wanafamilia wengine. Nimewatembelea wazazi na marafiki wenye wasisiwasi na kuvunjika moyo wa kijana aliyekuwa amejawa na matumaini ambaye alijiua. Nimehisi huzuni ya kiungu ya wale ambao wametenda dhambi na kwa dhati kutaka kutubu na madhara ya kutisha kwa wale walioathiriwa na dhambi.
Nimeona kuvunjika moyo kwa ambaye anateseka na ugonjwa wa akili na kwa wale wanaoteseka kimya kimya wakati wakimtazama bila ya kuwa na cha ziada cha kufanya kwenye hilo. Nimeona upotevu mkubwa uliosababishwa na majanga ya asili, mafuriko, dhoruba, moto, na matetemeko ya ardhi. Nimeshuhudia msukosuko katika nchi mbalimbali kutokana na dhoruba za kisiasa, vita, na maangamizo, na maumivu yanayokuja wakati yasiyotarajiwa yanapowekwa juu ya wale ambao hawana hatia na wanaotafuta kutenda yaliyo mema.
Mikono ya Uponyaji, na Kolby Larsen, isinakiliwe
Mwokozi Hutusaidia
Katika kuzungumzia kuhusu Upatanisho wa Yesu Kristo, Rais James E. Faust (1920–2007), Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza, alisema: "Waliojeruhiwa wanapaswa kufanya kile wanachoweza kufanya kushinda majaribu yao, na Mwokozi ‘atawasaidia watu wake kulingana na unyonge wao’ [Alma 7:12]. Yeye atatusaidia kubeba mizigo yetu. Baadhi ya majeraha yanaumiza sana na ni ya kina kiasi kwamba hayawezi kuponywa bila msaada kutokana na nguvu za juu na matumaini ya haki kamilifu na urejeshwaji katika maisha yajayo. … Yeye anaelewa maumivu yetu na atatembea pamoja nasi hata katika saa zetu za kiza."
Ninahisi kuzidi kuvutwa kwenye upendo wa Mwokozi na baraka zisizo na mwisho tulizoahidiwa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo. Hakutukinga dhidi ya uzoefu mgumu wa maisha ambao unaleta maumivu yasiyopimika, lakini alitulinda kutokana na mateso yasiyo na mwisho na utenganishwaji toka kwa Baba wa Mbinguni na kuturuhusu, kupitia mateso Yake ya kila aina, kuwa na uwezekano wa shangwe kamilifu na furaha ya milele katika uwepo wa Mungu.
Rais Dallin H. Oaks alitukumbusha: "Kwa upana zaidi, msaada wa Mungu wenye nguvu zaidi duniani ulikuwa ni utoaji Wake wa Mwokozi, Yesu Kristo, ambaye angeteseka kulipia gharama na kutoa msamaha wa dhambi ambazo zimefanyiwa toba. Upatanisho huo wa rehema na utukufu unaelezea kwa nini imani katika Bwana Yesu Kristo ni kanuni ya kwanza ya injili. Upatanisho Wake ‘huleta ufufuko wa wafu’ (Alma 42:23), na ‘unalipia dhambi za ulimwengu’ (Alma 34:8), hufuta dhambi zetu zote tulizotubu na kumpa Mwokozi wetu uwezo wa kutusaidia katika udhaifu wetu wa duniani."
Maelezo kutoka Sala huko Gethsemane, na Del Parson, yanaweza kunakiliwa kwa ajili ya matumizi ya Kanisa pekee
Tukio Muhimu la Umilele
Ninapofikiria mateso ambayo mimi binafsi nimeyaona, ambayo ni madogo sana ikilinganishwa na ya wote waliopo au watakaokuwepo duniani, siwezi, kwa maneno yoyote ninayoyajua, kuelezea hisia moyoni mwangu kwa kile ambacho lazima kimehisiwa moyoni na akilini na mwilini na nafsini mwa Mwokozi katika nyakati Zake takatifu za mateso ya aina yote kwa sababu ya dhambi na maumivu ya wanadamu wote.
Tukio muhimu la milele yote lilianza wakati Yesu akienda "mahali paitwapo Gethsemane" (Mathayo 26:36) katika Mlima wa Mizeituni nje ya kuta za mji wa Yerusalemu. Yeye aliwaambia wanafunzi Wake, "Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa" (Mathayo 26:38).
Yeye alisali, akisema, "Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe." (Mathayo 26:39). Yeye alirudi kwa wanafunzi Wake, akawakuta wamelala, akaondoka tena, na kusali mara ya pili. "Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. … Na [Yeye] akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale" (Mathayo 26:42, 44).
Yesu alikunywa kikombe kichungu na aliteseka katika bustani na msalabani zaidi ya tunavyoweza kuelewa. Akiwa hana dhambi, alijichukulia juu Yake dhambi zetu zote, kwamba tunapomwendea na kutubu, dhambi na mizigo yetu huondolewa kutoka kwetu (ona 2 Wakorintho 5:21).
Mateso ya Yesu, kifo, na dhabihu ya upatanisho kwa muda mrefu vilikuwa vimetarajiwa. Akizungumza miaka 700 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, Isaya alitoa unabii kwamba "Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote." (Isaya 53:6). Yesu alizungumzia kuutoa uhai Wake kama "fidia" (Mathayo 20:28; ona pia 1 Timotheo 2:6) "kwa ajili ya ondoleo la dhambi" (Mathayo 26:28) kwa ajili ya wote ambao wangemwamini na kutubu dhambi zao. Petro alielezea jinsi Yeye "alivyoteseka kwa ajili ya dhambi [zetu]" (1 Petro 3:18), kwamba kupitia kwa kupigwa Kwake tunaponywa (ona 1 Petro 2:24). Alifanya kile ambacho hakuna mwingine angeweza kukifanya ili kuturuhusu kurudi katika uwepo wa Baba yetu. Yeye "alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu" (Isaya 53:5).
Kufuatia mateso huko Gethsemane, maumivu Yake yaliendelea—kusalitiwa na mtu aliyetembea pamoja Naye, kejeli mbele ya watawala wasio na haki, maumivu mwilini Mwake wakati akipigwa, taji la miiba likilazimishwa kichwani Mwake na askari wakatili na wasio na huruma (ona Yohana 18:2–3, 12–14; Marko 15:15–20), na boriti nzito ikiwekwa juu ya nyama iliyochanika ya mgongo Wake alipokuwa akielekea Golgotha (ona Yohana 19:16–17).
Msalabani, maumivu makali yaliyokithiri kule Gethsemane yalikuwa na ukali ambao hakuna mwanadamu angeweza kuvumilia. Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, alijitwika agizo takatifu la Baba Yake la kutoa maisha Yake. Askari na watawala hawakuweza kulichukua kutoka Kwake (ona Yohana 10:18). Kwa heshima na unyenyekevu, Yesu aliinamisha kichwa Chake na kusema, "Imekwisha" (Yohana 19:30).
Wakati wa mwisho wa maisha Yake duniani ulikuwa umemalizika. Hakuna maneno ya kuelezea ukubwa wa hii zawadi Yake ya thamani. Kamwe haitahitajika kutoka kwa mwingine. Yesu Kristo aliteseka "mara moja tu" (Waebrania 10:10).
Amefufuka!
Pamoja na kazi Yake takatifu kutimizwa, Yeye sasa angekuwa wa kwanza katika historia yote ya mwanadamu kuinuka kutoka kaburini hadi kwenye kutokufa (ona 1 Wakorintho 15:21–23).
Kwa wanawake kaburini, malaika walisema:
"Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?
"Hayupo hapa, amefufuka" (Luka 24:5–6).
Kwa Mitume Wake, Yeye alisema, "Tazama mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe" (Luka 24:39). Baadaye, "alionekana [kwa zaidi ya] watu mia tano … kwa mara moja" (1 Wakorintho 15:6). Mashahidi walimwona Mwokozi aliyefufuka. Yeye hakuwa mfu. Yeye alikuwa hai.
Yesu Kristo alivunja minyororo na kamba za utumwa usio na mwisho wa kifo kwa ajili ya kila mtu aliyeishi au atakayeishi duniani (ona 1 Wakorintho 15:22). Alimshinda adui yetu anayetuzunguka pande zote; adui kifo milele alishindwa.
Rais Russell M. Nelson (1924–2025) alisema: "Yesu Kristo alijichukulia juu Yake dhambi zako , maumivu yako , huzuni yako kubwa, na udhaifu wako . Huna haja ya kuyabeba peke yako! Yeye atakusamehe unapotubu. Yeye atakubariki na kile unachohitaji. Yeye ataponya nafsi yako iliyojeruhiwa. Unapojifunga nira Kwake, mizigo yako itaonekana kuwa miepesi. Kama utafanya na kushika maagano ya kumfuata Yesu Kristo, utagundua kwamba nyakati za uchungu za maisha yako ni za muda. Mateso yako yatamezwa katika shangwe ya Kristo’ [Alma 31:38]"
Kama mmoja wa Mitume Wake waliotawazwa, nimepata uzoefu wa nyakati za kiroho na za binafsi ambazo zimeniletea ushuhuda wa uhakika na kweli kwamba Yeye yu hai. Katika msimu huu wa Pasaka, na maneno haya kwa upole yakae akilini na mioyoni mwetu: "Mwokozi sitasahau, Ulivyosulubiwa," wakati tunapofurahia katika kuimba:
© 2026 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya Tafsiri : 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, April 2026. Swahili. 20038 743