“Nitawaponya,” Liahona, Feb. 2025.
Ujumbe wa kila mwezi wa Liahona , Februari 2025.
“ Nitawaponya ”
Huduma ya uponyaji ya Mwokozi ni mwanzo mtakatifu na ahadi ya uponyaji wa kudumu wa kimwili na kihisia ambao utakuja kwa kila mmoja wetu katika Ufufuko.
Bado nakumbuka wazi baadhi ya safari ndefu za ndege nilizofanya wakati wa kazi yangu kama rubani wa ndege.
Katika mojawapo, ningeondoka Ujerumani saa 5 asubuhi na kutua California saa 7 mchana siku hiyo hiyo. Kulinganisha muda wa kuondoka na kuwasili, ingeonekana kwamba safari kuvuka Bahari ya Atlantiki na bara la Amerika Kaskazini ilichukua saa mbili tu. Boeing 747 ilienda kasi, lakini siyo kasi hivyo! Kiuhalisia, ilituchukua karibu saa 11, ikitegemea upepo, kusafiri maili 5,600 (kilomita 9,000).
Kwa sababu tulikuwa tunasafiri kuelekea magharibi, jua kamwe halikutua wakati wa safari yetu. Tulikuwa tukifurahia mwangaza wa siku njia nzima kutokea Ujerumani hadi California.
Kurudi Ujerumani, hata hivyo, ilikuwa hadithi nyingine tofauti. Hata wakati tulipoondoka mapema mchana, tuliposafiri kuelekea mashariki, machweo ya jua yalifika upesi sana kuliko kawaida, na bila kujua, usiku ulitufikia.
Wakati wa hizi safari ndefu, nafsi yangu ilijawa na mshangao nilipotafakari uzuri wa dunia hii na utaratibu wa uumbaji wa Mungu. Hata kusafiri usiku, katika giza totoro, nilijua kwa hakika kwamba jua lingepambazuka tena, kwamba mwanga angavu ungerudi na kuleta joto na maisha ya siku mpya kabla ya mwisho wa safari yetu. Hali ya safari yangu ingeweza kuwa ilifanya jua lionekane kutua pole pole sana au upesi sana, lakini nilijua kwamba jua lilibaki imara, thabiti, na la kutegemewa katika mbingu.
Ninahisi vivyo hivyo kuhusu Mungu. Kwa sababu nina uhakika uliojikita kwa kina wa hekima ya Mungu na kusudi la uumbaji Wake wote, ninaweza kuhisi tumaini la shangwe na amani ya kudumu ninapofikiria kuhusu maisha yetu ya duniani. Sisi ni watoto wa Mungu. Yeye anatupenda. Yeye anajua hali zetu. Yeye yu tayari kusaidia. Kweli hizi hazibadiliki, hata wakati mambo mengine yanayotuzunguka yanapooneka kutokuwa thabiti na yasiyotabirika.
Sisi sote tunapitia nyakati za giza, huzuni na wasiwasi ambao unatishia amani yetu. Nina shukrani iliyoje kwa ajili ya chanzo thabiti na cha kweli cha ukweli na nuru (ona Mafundisho na Maagano 88: 6–11). Yesu Kristo ndiye nuru na uzima wa ulimwengu. Kwa sababu yake Yeye na dhabihu Yake ya kulipia dhambi, tunalo tumaini kwa ajili ya siku za usoni, kupata njia ya kufikia nuru takatifu ili kuangaza siku za giza za safari yetu, na ahadi ya ushindi wa mwisho juu ya dhambi na kifo.
“Yeye Anaupenda Ulimwengu”
Yesu Kristo alikuwa ndiye mtu pekee mkamilifu aliyewahi kutembea duniani. Kwa sababu ya maisha Yake makamilifu, Yeye hakudaiwa na haki. Kutokana na upendo kwetu, Yeye aliutoa uhai Wake kwa ajili ya kila mmoja wetu binafsi na kwa ajili ya watoto wote wa Mungu kwa pamoja ili kufungua mlango wa kutokufa na uzima wa milele.
Licha ya kile ambacho Shetani angetaka sisi tuamini, hakuna yeyote kati yetu aliye mbali na uwezo wa Mwokozi wa kutuokoa. Hakuna yeyote kati yetu asiyestahili neema ya msamaha. Hakuna yeyote kati yetu aliye mbali na “kuzingirwa milele katika mikono ya upendo wake” (2 Nefi 1:15).
Zawadi hii kuu kuliko zawadi zote huja kutokana na nguvu wezeshi na za kukomboa za Upatanisho wa Yesu Kristo. Kwa sababu ya kuteseka kwa Mwokozi katika Gethsemane na huko Golgotha, Yeye anajua jinsi ya kutuokoa sisi na kutusaidia kushinda udhaifu wetu wote (ona Alma 7:12).
“Yeye hafanyi chochote ila tu kwa manufaa ya ulimwengu; kwani anaupenda ulimwengu, hata kwamba anatoa maisha yake ili awavute wanadamu wote kwake” (2 Nefi 26:24).
Yesu Kristo ni nguvu yetu!
Yeye hutufikia.
Yeye hurejesha.
Yeye huokoa.
“Wakati Mwokozi [alipotoa dhabihu Yake ya kulipia dhambi] kwa ajili ya wanadamu wote, Yeye alifungua njia ambayo wale wanaomfuata wanaweza kufikia uwezo Wake wa uponyaji, uimarishaji na ukombozi,” alisema Rais Russell M. Nelson.
Nguvu hiyo, kama vile jua, daima ipo hapo. Kamwe haiyumbi. Uchaguzi wa kufuata katika nyayo za Mwokozi ni kama kutembea nje ya vivuli na katika mwanga wa jua, ambapo tunaweza kupokea baraka za nuru, joto na upendo wa Mungu. Ninajua kwamba siku moja, tutatazama nyuma na kujawa na shukrani kwamba tulifanya uamuzi muhimu wa milele wa kumtumaini Yesu Kristo na upendo Wake wa kiungu wenye kutuinua na kutuimarisha sisi.
“Rudini Kwangu”
Kitabu cha Mormoni husimulia juu ya watu ambao walitumia siku tatu katika giza totoro kufuatia Kusulubiwa kwa Mwokozi. Giza halisi kuwazunguka wao lingeashiria giza la kiroho sisi sote tunalopitia kwa sababu ya dhambi. Kisha watu wale walisikia sauti ya Kristo akiwaalika wao watoke gizani na kuja kwenye nuru Yake:
“Je, mtarudi kwangu sasa, na kutubu dhambi zenu, na kugeuka ili niwaponye?” (3 Nefi 9:13)
“Na mtatoa kwangu dhabihu ya moyo uliopondeka na roho iliyovunjika” (3 Nefi 9:20).
“Mtatubu na kunirudia kwa lengo moja la moyo” (3 Nefi 10:6).
Mwokozi anatoa mialiko hiyo hiyo kwetu leo wakati tunapojikuta tumepotea gizani. Kama vile kila mawio ya jua yanavyoashiria kuanza kwa siku mpya, kila wakati tunapotubu, tunapokea mwanzo mpya, mwanzo mpya angavu.
Hiyo haimaanishi kwamba ni rahisi. Toba humaanisha mabadiliko, na mabadiliko hayatokei upesi. Wakati toba ya shangwe, inajumuisha “huzuni ya kimungu” (2 Wakorintho 7:10). Inatuhitaji kwamba tukubali na kukiri makosa yetu, kuomba msamaha kutoka kwa Mungu na kutoka kwa wale ambao yawezekana kuwa tuliwaumiza. Zaidi ya yote, huhitaji kwamba tutafute “Roho wa Bwana Mwenyezi,” kwamba tupate “mabadiliko makuu … mioyoni mwetu, hata kwamba hatuna tamaa ya kutenda maovu tena, lakini kutenda mema daima” (Mosia 5:2).
Aina hiyo ya mabadiliko ni safari ndefu, lakini punde unapopiga hatua ya kwanza “siku ya wokovu wako” inaanza, na “mara moja mpango mkuu wa ukombozi unatimizwa kwako” (Alma 34:31).
Kupitia toba yetu ya dhati, Mungu anaahidi kutusamehe na kutozikumbuka tena dhambi zetu. Tunapokuwa na wakati mgumu kusahau dhambi zetu, acha tujitahidi kuamini katika ahadi ya Bwana ya kusamehe na kujifunza kuwasamehe wengine na kujisamehe sisi wenyewe.
“Roho zetu zinaharibiwa wakati tunapofanya makosa na kutenda dhambi,” alifundisha Rais Boyd K. Packer (1924–2015). “Lakini tofauti na miili yetu ya duniani, wakati mchakato wa toba unapokamilika, hakuna makovu yanayobaki kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo.”
Kuponywa kwa Mtu Asiyeona, na Carl Heinrich Bloch
“Waleteni Hapa”
Mwokozi ni Mponyaji Mkuu. Mojawapo ya maonesho mazuri sana ya nguvu Zake za uponyaji hupatikana katika Kitabu cha Mormoni, katika hadithi ya huduma Yake ya ana kwa ana katika Amerika ya kale:
“Mnao wowote ambao ni wagonjwa miongoni mwenu?” Yeye aliwauliza. “Waleteni hapa. Mnao wowote ambao ni viwete, au vipofu, au wa kupooza, au vilema, au wenye ukoma, au walionyauka au ni viziwi, au ambao wanateseka kwa njia yoyote? Waleteni hapa na nitawaponya, kwani ninayo huruma juu yenu; matumbo yangu yamejawa na huruma. …
“Na ikawa kwamba wakati alipokuwa amesema hivyo, umati wote, kwa lengo moja, ulisonga mbele na wagonjwa wao na walio sumbuka wao, na vilema wao, na vipofu wao, na bubu wao, na wote walio sumbuka kwa jinsi yoyote; na akawaponya kila mmoja vile walivyoletwa kwake” (3 Nefi 17:7, 9).
Kila wakati Mwokozi alipomponya mtu yeyote, “waliosumbuka kwa jinsi yoyote,” kabla na baada ya Ufufuko Wake, ilikuwa ni ushuhuda wa uwezo Wake mkuu wa kuponya nafsi zetu. Kila uponyaji wa miujiza ulikuwa ni mwanzo na ahadi ya uponyaji wa kudumu wa kimwili na kihisia ambao utakuja kwa kila mmoja wetu katika Ufufuko, ambao “ni tendo kamili la Bwana la uponyaji.”
Ni kweli kwamba sala zetu kwa ajili ya uponyaji katika maisha haya si mara zote hujibiwa katika njia tunayotumainia, lakini kamwe hazipuuzwi. Wakati wa uponyaji utafika, kama vile ambavyo giza la usiku daima huondoka—katika wakati mwafaka—kwa mawio matukufu.
Kama vile Rais Nelson ambavyo ameshuhudia: “Imani yetu kamwe haidharauliwi. Najua kuwa mtazamo wa Baba yetu wa Mbinguni ajuaye yote ni mpana sana kuliko wetu. Wakati tukijua matatizo yetu ya maisha ya duniani na maumivu, Yeye anajua maendeleo yetu kuelekea maisha ya milele na uwezekano wetu wa kuwa. Kama tutasali ili kujua mapenzi Yake na kujiweka chini yake kwa subira na ujasiri, uponyaji wa kimbingu unaweza kufanyika katika njia Yake na wakati Wake.”
Hivi karibuni mimi na mke wangu, Harriet, tulijumuisha katika sala zetu tumaini maalumu na kusihi kwa niaba ya baadhi ya tunaowapenda. Tulisali kwamba timu yao ya huduma ya afya ingeweza kupatiwa uwezo mahususi wa kutibu maradhi yao. Tulipata msukumo wa kuongeza kwamba hata kama tiba ya haraka au nafuu ya haraka havingeweza kutokea, nguvu ya Mwokozi ya uponyaji ingewaletea faraja na amani. Matokeo ya uponyaji wa nguvu ya ukombozi ya Mwokozi yanaweza hata kuwa na matokeo makubwa zaidi kwenye afya yetu ya kihisia, kiroho na hata kimwili kuliko tiba yoyote ya kidunia tunayoweza kupokea. Yesu Kristo ndiye Mponyaji katika maisha haya na katika milele.
Kaka zangu na dada zangu, marafiki wapendwa, ninashuhudia kwamba rehema za Mwokozi wetu zinatosha kuponya vidonda vyetu, kukusafisha dhambi, kukuimarisha wewe kwa ajili ya majaribu yatakayokuja, na kukubariki uwe na tumaini, hekima na amani Yake. Nguvu Zake daima zipo—thabiti na za kutegemewa—hata wakati sisi, kwa muda, tunahisi kuwa mbali na upendo, nuru na joto Lake.
Ninaomba kamwe tusipoteze hisia zetu za heshima kuu na shukrani kubwa kwa ajili ya yote ambayo Yesu Kristo amefanya kwa ajili yetu. Tafadhali jua kwamba wewe unapendwa kikamilifu, na kumbuka kile ambacho umeahidiwa milele.
“Mungu na awawezeshe kwamba mizigo yenu ipate kuwa miepesi, kupitia shangwe inayotokana na Mwanawe,” Yesu Kristo (Alma 33:23).
© 2025 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa huko Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, February 2025. Swahili. 19609 743