“2. Kuwasaidia Watu Binafsi na Familia katika Kazi ya Mungu ya Wokovu na Kuinuliwa,” Kurasa Zilizochaguliwa kutoka kwenye Kitabu cha Maelezo ya Jumla (2013).
“2. Kuwasaidia Watu Binafsi na Familia,” Kurasa Zilizochaguliwa kutoka kwenye Kitabu cha Maelezo ya Jumla
2.
Kuwasaidia Watu Binafsi na Familia katika Kazi ya Mungu ya Wokovu na Kuinuliwa
2.0
Utangulizi
Kama kiongozi katika Kanisa la Yesu Kristo, unawasaidia watu binafsi na familia katika kutimiza kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa (ona 1.2). Hatima ya lengo la kazi hii ni kuwasaidia watoto wote wa Mungu wapokee baraka za uzima wa milele na utimilifu wa shangwe.
Kazi nyingi za Mungu za wokovu na kuinuliwa zinakamilishwa kupitia familia. Kwa waumini wote wa Kanisa, kiini cha kazi hii ni nyumbani.
2.1
Wajibu wa Familia katika Mpango wa Mungu
Kama sehemu ya mpango Wake, Baba wa Mbinguni ameanzisha familia duniani. Anakusudia familia zituletee furaha. Familia zinatoa fursa ya kujifunza, kukua, kuhudumu, kutubu, na kusamehe. Zinaweza kutusaidia tujiandae kwa ajili ya uzima wa milele.
Ahadi ya Mungu ya uzima wa milele inajumuisha ndoa ya milele, watoto, na baraka zingine zote za familia ya milele. Ahadi hii inatumika kwa wale ambao kwa sasa hawajaoa au hawajaolewa au wasio na familia katika Kanisa.
2.1.1
Familia za Milele
Familia za milele zinaundwa wakati waumini wa Kanisa wanapofanya maagano pale wanapopokea ibada za kuunganishwa ndani ya hekalu. Baraka za familia ya milele huja pale waumini wanaposhika maagano hayo na kutubu wakati wanapokosea. Viongozi wa Kanisa wanawasaidia waumini wajiandae kupokea ibada hizi na kuheshimu maagano yao.
Kipengele cha ziada cha kuanzisha familia za milele ni kufanya ibada katika hekalu zinazowaruhusu waumini kuunganishwa kwa mababu zao waliofariki.
2.1.2
Mume na Mke
Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke imetakaswa na Mungu (ona Mafundisho na Maagano 49:15). Mume na mke wanakusudiwa kuendelea kukua pamoja kuelekea uzima wa milele (ona 1 Wakorintho 11:11).
Moja ya vigezo kwa ajili ya kupata uzima wa milele ni kwa mwanamume na mwanamke kuingia katika agano la ndoa ya milele (ona Mafundisho na Maagano 131:1–4). Wanandoa wanafanya agano hili wakati wanapopokea ibada ya kuunganishwa katika ndoa ndani ya hekalu. Agano hili ni msingi wa familia ya milele. Likitunzwa kwa uaminifu, linaruhusu ndoa yao kudumu milele.
Mahusiano ya kimapenzi kati ya mume na mke yanakusudiwa kuwa ya kupendeza na matakatifu. Yameamriwa na Mungu kwa ajili ya uumbaji wa watoto na kwa ajili ya kuonyesha upendo kati ya mume na mke. Upole na heshima—siyo ubinafsi—vinapaswa kuongoza uhusiano wao wa kimapenzi.
Mungu ameamuru kuwa kujamiiana kuhifadhiwe kwa ajili ya ndoa kati ya mwanamume na mwanamke.
Mume na mke wako sawa machoni pa Mungu. Mmoja hapaswi kumtawala mwingine. Maamuzi yao yanapaswa kufanywa kwa umoja na upendo, pamoja na ushiriki mkamilifu wa wote.
2.1.3
Wazazi na Watoto
Manabii wa siku za mwisho wamefundisha kwamba “amri ya Mungu kwa watoto Wake ya kuongezeka na kuijaza dunia inabaki kuwa na nguvu” (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”; ona pia Mafundisho na Maagano 49:16–17).
Mume na mke wenye upendo kwa pamoja wanaweka mazingira yaliyo bora zaidi kwa ajili ya kuwalea na kuwafunza watoto. Hali binafsi zinaweza kuwazuia wazazi kuwalea watoto wao kwa pamoja. Hata hivyo, Bwana atawabariki wanapotafuta msaada Wake na wanapojitahidi kutunza maagano yao pamoja Naye.
Wazazi wana jukumu muhimu la kuwasaidia watoto wao wajiandae kupokea baraka za uzima wa milele. Wanawafundisha watoto wao kumpenda na kumtumikia Mungu na wengine (ona Mathayo 22:36–40).
“Akina baba wanapaswa kusimamia familia zao katika upendo na haki na wana jukumu la kukimu mahitaji ya maisha na ulinzi kwa familia zao” (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”). Wakati panapokuwa hakuna mume au baba katika nyumba, mama anaongoza katika familia.
Kuongoza katika familia ni jukumu la kusaidia kuwaongoza wanafamilia kurudi kuishi katika uwepo wa Mungu. Hii inafanyika kwa kuhudumu na kufundisha kwa upole, unyenyekevu, na upendo msafi, kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo (ona Mathayo 20:26–28). Kuongoza katika familia kunajumuisha kuwaongoza wanafamilia katika sala za kila siku, kujifunza injili, na vipengele vingine vya kuabudu. Wazazi wanafanya kazi kwa umoja ili kutimiza majukumu haya.
“Akina mama wana jukumu la kimsingi kwa utunzaji wa watoto wao” (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”). Kutunza maana yake ni kustawisha, kufundisha, na kuunga mkono, kwa kufuata mfano wa Mwokozi (ona 3 Nefi 10:4). Katika umoja na mume wake, mama anasaidia familia yake kujifunza kweli za injili na kujenga imani kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Kwa pamoja wanakuza mazingira ya upendo katika familia.
“Katika majukumu haya matakatifu, akina baba na akina mama wana wajibu wa kusaidiana wao kwa wao kama washiriki sawa” (“Familia: Tangazo kwa Ulimwengu”). Kwa sala wanashauriana pamoja na pia na Bwana.
2.2
Kazi ya Mungu ya Wokovu na Kuinuliwa Nyumbani
Urais wa Kwanza ulisema, “Nyumbani ni msingi wa maisha ya uadilifu” (First Presidency letter, Feb. 11, 1999).
Ili kuwasaidia waumini katika kufanya kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa nyumbani, viongozi wa Kanisa wanawahimiza kuweka nyumba zao kuwa mahali ambapo Roho yupo. Pia wanawahimiza waumini kuheshimu siku ya Sabato, kujifunza na kusoma injili nyumbani, na kufanya jioni ya nyumbani kila wiki.
2.2.3
Kujifunza na Kusoma Injili Nyumbani
Kufundisha na kujifunza injili ambako kiini chake ni nyumbani na kusaidiwa na Kanisa. Viongozi wa Kanisa wanawahimiza waumini wote kujifunza injili nyumbani siku ya Sabato na katika wiki yote.
Mafunzo ya maandiko kama yalivyoelezwa kwa muhtasari kwenye Njoo, Unifuate ni kozi iliyopendekezwa ya kujifunza injili nyumbani.
2.2.4
Jioni ya Nyumbani na Shughuli Nyinginezo
Manabii wa siku za mwisho wamewashauri waumini wa Kanisa kuwa na jioni ya nyumbani kila wiki. Huu ni muda mtakatifu kwa ajili ya watu binafsi na familia kujifunza injili, kuimarisha shuhuda, kujenga umoja, na kuwa na furaha wao kwa wao.
Jioni ya nyumbani inaweza kubadilika kulingana na hali za waumini. Inaweza kufanyika siku ya Sabato au siku na muda mwingine. Inaweza kujumuisha:
-
Mafunzo na maelekezo ya injili (nyenzo za Njoo, Unifuate zinaweza kutumika kulingana na mapendeleo).
-
Kuwatumikia wengine.
-
Kuimba au kupiga nyimbo za Kanisa na nyimbo za Watoto (ona sura ya 19).
-
Kuwasaidia wanafamilia katika Maendeleo ya Watoto na Vijana.
-
Baraza la familia la kuweka malengo, kutatua matatizo, na kuratibu ratiba.
-
Shughuli za burudani.
Waumini waseja na wengine wanaweza kukusanyika katika vikundi katika muda tofauti na ibada za kuabudu za Sabato ili kushiriki katika jioni ya nyumbani na kuimarishana kupitia kujifunza injili.
2.2.5
Kuwasaidia Watu Binafsi
Viongozi wa Kanisa wanawasaidia waumini wanaohitaji msaada wa ziada wa kifamilia. Viongozi wanawasaidia waumini hawa na familia zao kuwa na fursa ya ushirika, uzoefu wa kijamii wenye siha, na ukuaji wa kiroho.
2.3
Uhusiano kati ya Nyumbani na Kanisani
Kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa kiini chake ni nyumbani na inasaidiwa na Kanisa. Kanuni zifuatazo zinatumika katika uhusiano kati ya Nyumbani na Kanisani.
-
Viongozi na walimu wanaheshimu wajibu wa wazazi na wanawasaidia.
-
Baadhi ya mikutano ya Kanisa ni muhimu katika kila kata au tawi. Hii inajumuisha mikutano ya sakramenti na madarasa na mikutano ya akidi inayofanywa siku ya Sabato. Mikutano mingine mingi, shughuli, na programu siyo muhimu.
-
Bwana atawabariki waumini wakati wanapohudumu na kutoa dhabihu katika Kanisa Lake. Hata hivyo, kiasi cha muda kilichotengwa kwa ajili ya huduma ya Kanisa hakipaswi kupunguza uwezo wa waumini kutimiza wajibu wao nyumbani, kazini, na sehemu nyingine.