“0. Muhtasari wa Utangulizi,” Kurasa Zilizochaguliwa kutoka kwenye Kitabu cha Maelezo ya Jumla (2023).
“0. Muhtasari wa Utangulizi,” Kurasa Zilizochaguliwa kutoka kwenye Kitabu cha Maelezo ya Jumla
0.
Muhtasari wa Utangulizi
0.0
Utangulizi
Bwana alifundisha, “acha kila mtu na ajifunze wajibu wake, na kutenda kazi katika ofisi ambayo ameteuliwa, kwa bidii yote” (Mafundisho na Maagano 107:99). Kama kiongozi katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, unapaswa kutafuta ufunuo binafsi ili ukusaidie kujifunza na kutimiza majukumu ya wito wako.
Kujifunza maandiko na mafundisho ya manabii wa siku za mwisho kutakusaidia uelewe na utimize majukumu yako. Unapojifunza maneno ya Mungu, utakuwa mpokeaji mzuri zaidi wa ushawishi wa Roho (ona Mafundisho na Maagano 84:85).
Pia unajifunza majukumu yako kwa kusoma maelekezo katika kitabu hiki cha maelezo. Maelekezo haya yanaweza kualika ufunuo kama yatatumika kutoa uelewa wa kanuni, sera, na taratibu za kutumia wakati unapotafuta mwongozo wa Roho.
0.1
Kitabu cha Maelezo ya Jumla
Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kinatoa mwongozo kwa ajili ya viongozi wakuu na viongozi wa Kanisa wa maeneo husika.
Vichwa vya habari na vichwa vidogo vya habari katika Kitabu hiki cha maelezo vimepewa namba ili kufanya mada ziwe rahisi kupatikana na kurejelea. Kwa mfano, maelekezo kuhusu nani anaweza kuunganishwa katika hekalu yametolewa katika 27.3.1. Namba 27 inahusu sura, namba 3 inahusu kipengele katika sura ile, na namba 1 inahusu kipengele kidogo.
0.2
Mabadiliko na Nyenzo za Hiari
Siyo vigingi na kata zote zina mahitaji yaliyo sawa.
Viongozi wanatafuta mwongozo wa kiungu kuhusu miongozo ipi na nyenzo zipi za hiari zitumike ili kukidhi mahitaji ya waumini.
0.4
Maswali kuhusu Maelekezo
Wakati maswali yanapotokea ambayo hayana majibu katika maandiko, maneno ya manabii walio hai, au kitabu hiki cha maelezo, waumini wa Kanisa wanapaswa kutegemea katika maagano yao na Mungu, ushauri wa viongozi wa maeneo yao, na mwongozo wa kiungu wa Roho kwa ajili ya kuwaongoza.
Kama viongozi wana maswali kuhusu taarifa katika kitabu hiki cha maelezo au kuhusu maswala ambayo majibu yake hayamo humu, washauriane na mamlaka kiongozi ya eneo lao.
0.5
Istilahi
Isipokuwa pale ilipoelekezwa vinginevyo:
-
Maneno askofu na uaskofu katika kitabu hiki cha maelezo yanahusu pia marais wa matawi na urais wa matawi. Maneno rais wa kigingi na urais wa kigingi yanahusu pia marais wa wilaya na urais wa wilaya. Kwa muhtasari juu ya jinsi gani mamlaka ya marais wa wilaya yanatofautiana na yale ya marais wa vigingi, ona 6.3.
-
Marejeleo kwa neno kata na vigingi kwa ujumla pia yanatumika kwa matawi, wilaya, na misheni.
-
Marejeleo kuhusu siku ya Jumapili yanatumika kwa siku yoyote ambayo sabato inaadhimishwa katika eneo husika.
-
Neno kitengo linahusu kata na matawi.
-
Marejeleo kuhusu wazazi kwa ujumla pia yanatumika kwa walezi kisheria.
Miito ya askofu na rais wa tawi hailingani katika mamlaka na wajibu, kadhalika miito ya rais wa kigingi na rais wa wilaya. Askofu ni ofisi katika ukuhani, na kutawazwa kwake kunaidhinishwa na Urais wa Kwanza tu. Marais wa vigingi huitwa na Viongozi Wakuu Wenye Mamlaka na Sabini wa Maeneo.
0.6
Kuwasiliana na Makao Makuu ya Kanisa au Ofisi ya Eneo
Baadhi ya sura katika kitabu hiki cha maelezo zinajumuisha maelekezo ya kuwasiliana na makao makuu ya Kanisa au ofisi ya eneo. Maelekezo ya kuwasiliana na makao makuu ya Kanisa yanahusu wale waliopo Marekani na Kanada. Maelekezo ya kuwasiliana na ofisi za eneo yanahusu wale waliopo nje ya Marekani na Kanada.