Maktaba
Kiambatisho


Kiambatisho

Baba yako wa Mbinguni anakualika kupokea ibada takatifu. Ibada hizi zinajumuisha maagano—unafanya ahadi na Mungu, na Yeye anafanya ahadi na wewe. Unafanya maagano haya, kwa mfano, wakati unapobatizwa na kuthibitishwa, unapopokea endaumenti, na wakati unapounganishwa kwa muda na milele yote katika nyumba ya Bwana. Kufanya na kushika maagano kutakuletea shangwe na furaha na kutakuruhusu wewe kufikia nguvu za Mungu ili kukusaidia kurudi katika uwepo Wake, mahali ambapo unaweza kufurahia uzima wa milele pamoja Naye.

Ili kujifunza zaidi kuhusu kile unachomwahidi Mungu unapofanya maagano haya—na kile Yeye anachoahidi kwako—ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 3.5, Maktaba ya Injili.

Tafakari maswali ya hapo chini. Ni maswali unayoulizwa unapohojiwa ili kupokea kibali cha hekaluni, lakini usingoje kwa ajili ya usaili. Fanya tathmini yako mwenyewe ya kiroho wakati wowote unapotaka kufanya hivyo.

Dhima ya Wasichana, Dhima ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni na zile Amri Kumi vinaweza pia kuwa nyenzo zenye msaada katika kujitathmini kwako binafsi.

Maswali ya Kibali cha Hekaluni kwa ajili ya Vijana

  • Je, una imani na ushuhuda juu ya Mungu, Baba wa Milele; Mwanaye, Yesu Kristo; na Roho Mtakatifu?

  • Je, una ushuhuda juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo na wa jukumu Lake kama Mwokozi na Mkombozi wako?

  • Je, unao ushuhuda juu ya Urejesho wa injili ya Yesu Kristo?

  • Je, unamkubali Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kama nabii, mwonaji na mfunuzi na kama mtu pekee duniani aliyepewa mamlaka ya kutumia funguo zote za ukuhani? Je, unawakubali washiriki wa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili kama manabii, waonaji na wafunuzi? Je, unawakubali Viongozi Wakuu wengine wenye Mamlaka na viongozi wa Kanisa wa eneo lako?

  • Bwana amesema kwamba mambo yote lazima “yafanyike katika usafi” mbele Yake (Mafundisho na Maagano 42:41). Je, unajitahidi kuwa msafi kimaadili katika mawazo na tabia zako? Je, unatii sheria ya usafi wa kimwili?

  • Je, unafuata mafundisho ya Kanisa la Yesu Kristo katika tabia yako faraghani na hadharani kwa washiriki wa familia yako na watu wengine?

  • Je, unaunga mkono au kutangaza mafundisho yoyote, matendo au kanuni zilizo kinyume na zile za Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa siku za Mwisho?

  • Je, unajitahidi kuitakasa siku ya Sabato, kote nyumbani na kanisani; kuhudhuria mikutano yako; kujiandaa na kupokea sakramenti kwa kustahili; na kuishi maisha yako sawa sawa na sheria na amri za injili?

  • Je, unajitahidi kuwa mwaminifu katika yote unayoyafanya?

  • Je, wewe ni mlipa zaka kamili?

  • Je, unaelewa na kutii Neno la Hekima?

  • Je, kuna dhambi nzito katika maisha yako ambazo zinahitaji kutatuliwa na mamlaka za ukuhani kama sehemu ya toba yako?

  • Je, unajiona kuwa ni mwenye kustahili kuingia katika nyumba ya Bwana na kushiriki katika ibada za hekaluni?

Dhima ya Wasichana

Mimi ni binti mpendwa wa wazazi wa Mbinguni, mwenye asili takatifu na hatima ya milele.

Kama mwanafunzi wa Yesu Kristo, ninajitahidi kuwa kama Yeye. Ninatafuta na kufanyia kazi ufunuo binafsi na kuwatumikia wengine katika jina Lake takatifu.

Nitasimama kama shahidi wa Mungu katika nyakati zote na katika vitu vyote na katika mahali popote.

Ninapojitahidi kuwa mwenye kustahili kuinuliwa, ninathamini zawadi ya toba na kutafuta kufanya vizuri zaidi kila siku. Kwa imani, nitaimarisha nyumba na familia yangu, kufanya na kushika maagano matakatifu, na kupokea ibada na baraka za hekalu takatifu.

Dhima ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni

Mimi ni mwana mpendwa wa Mungu na Yeye anayo kazi ya kufanywa na mimi.

Kwa moyo, uwezo, akili na nguvu zangu zote, nitampenda Mungu, nitashika maagano yangu na kutumia ukuhani Wake ili kuwatumikia wengine, nikianzia nyumbani mwangu mwenyewe.

Ninapojitahidi kuhudumu, kutumia imani, kutubu na kufanya vizuri zaidi kila siku, nitastahili kupokea baraka za hekaluni na shangwe ya kudumu ya injili.

Nitajitayarisha kuwa mmisionari mwenye juhudi, mume mwaminifu na baba mwenye upendo kwa kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo.

Nitasaidia kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya kurudi kwa Mwokozi kwa kuwaalika wote kuja kwa Kristo na kupokea baraka za Upatanisho Wake.

Amri Kumi

  • Usiwe na miungu mingine ila mimi.

  • Usijifanyie sanamu yoyote ya kuchonga.

  • Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako.

  • Ikumbuke siku ya sabato, na kuitakasa.

  • Waheshimu baba yako na mama yako.

  • Usiue.

  • Usizini.

  • Usiibe.

  • Usishuhudie uongo.

  • Usitamani.

Ona Kutoka 20:3–17.