Njoo, Unifuate
Kiambatisho C: Kwa ajili ya Msingi—Maelekezo kwa Ajili ya Muda wa Kuimba na Mawasilisho ya Watoto Kwenye Mkutano wa Sakramenti


“Kiambatisho C: Kwa ajili ya Msingi—Maelekezo kwa Ajili ya Muda wa Kuimba na Mawasilisho ya Watoto Kwenye Mkutano wa Sakramenti,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Agano la Kale 2026 (2026)

“Kiambatisho C,” Njoo, Unifuate: Agano la Kale 2026

watoto wakiimba

Kiambatisho C

Kwa Ajili ya Msingi—Maelekezo kwa Ajili ya Muda wa Kuimba na Mawasilisho ya Watoto Kwenye Mkutano wa Sakramenti

Muziki mtakatifu ni zana yenye nguvu katika kuwasaidia watoto wajifunze kuhusu mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni na kweli za msingi za injili ya Yesu Kristo. Wakati watoto wanapoimba kuhusu kanuni za injili, Roho Mtakatifu atashuhudia juu ya ukweli wa kanuni hizo. Maneno na muziki vitakaa katika akili na mioyo ya watoto maisha yao yote.

Tafuta msaada wa Roho unapojiandaa kufundisha injili kupitia muziki. Toa ushuhuda wako juu ya kweli hizo mnazoziimba. Wasaidie watoto waone jinsi muziki unavyohusiana na kile wanachopitia na kujifunza nyumbani na katika madarasa ya Watoto.

Miongozo kwa ajili ya Mawasilisho Kwenye Mkutano wa Sakramenti

Kwa maelekezo ya askofu, mawasilisho ya watoto kwenye mkutano wa sakramenti kwa kawaida hufanyika katika robo ya nne ya mwaka. Kama urais wa Msingi na kiongozi wa muziki, fanyeni kazi pamoja na mshauri katika uaskofu mwenye kusimamia Msingi ili kuanza kupanga mawasilisho.

Uwasilishaji sharti uwaruhusu watoto kuwasilisha kile ambacho wao na familia zao wamejifunza kutoka kwenye Agano la Kale nyumbani na katika darasa la Watoto, ikijumuisha nyimbo za Watoto walizoimba katika kipindi cha mwaka mzima. Wakati mkipanga mawasilisho, fikirieni njia ambazo mawasilisho hayo yanaweza kusaidia mkusanyiko kufokasi juu ya Mwokozi na mafundisho Yake.

Matawi yenye idadi ndogo ya watoto yanaweza kufikiria njia ambazo wanafamilia wanaweza kushiriki pamoja na watoto wao. Mshiriki wa uaskofu anaweza kuhitimisha mkutano kwa hotuba fupi.

Wakati ukiandaa mawasilisho, kumbuka miongozo ifuatayo:

  • Mazoezi yasichukue muda usio wa lazima kutoka kwenye madarasa ya Msingi au familia.

  • Vitu vya kutazama, mavazi maalumu na mawasilisho ya kimtandao havifai kwa ajili ya mkutano wa sakramenti.

Ona Kitabu cha Maelekezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 12.2.1.2, Maktaba ya Injili.

watoto wakiimba

Maelekezo kwa ajili ya Muda wa Kuimba

Dakika 5 (Urais wa Msingi): Sala ya kufungua, andiko au makala ya imani, na hotuba moja

Dakika 20 (kiongozi wa muziki): Muda wa kuimba

Urais wa Msingi na kiongozi wa muziki huchagua nyimbo kwa ajili ya kila mwezi ili kuimarisha kanuni ambayo watoto wanajifunza katika madarasa yao na nyumbani. Orodha ya nyimbo ambazo zinaimarisha kanuni hizi imejumuishwa katika mwongozo huu.

Unapofundisha nyimbo kwa watoto, waalike waeleze kile ambacho tayari wamejifunza kuhusu hadithi na kanuni za mafundisho zilizoko kwenye nyimbo. Waalike watoto watoe mawazo na hisia zao kuhusu kweli zinazopatikana katika nyimbo.

Kitabu cha Nyimbo za Watoto ni nyenzo ya muhimu kwa ajili ya muziki katika Msingi. Nyimbo kutoka katika kitabu cha nyimbo za dini na nyimbo kutoka kwenye jarida la Rafiki pia ni sahihi. Unaweza pia kutumia nyimbo kutoka Nyimbo za Dini—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani. Matumizi ya muziki mwingine wowote katika Msingi lazima yaidhinishwe na uaskofu (ona Kitabu cha Maelekezo ya Jumla, 12.3.4).

Muziki kwa ajili ya Muda wa Kuimba

Januari

  • My Heavenly Father Loves Me,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 228–29

  • I Will Follow God’s Plan,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 164–65

Februari

  • Follow the Prophet,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 110–11

  • A Child’s Prayer,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 12–13

Machi

  • Kindness Begins with Me,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,145

  • Ninakuhitaji,” Nyimbo za Dini, no. 47

Aprili

  • Gethsemane,” Gospel Library

  • Keep the Commandments,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 146

Mei

  • “Mahali Patakatifu,” Maktaba ya Injili

  • Nisomapo Maandiko,” Nyimbo za Dini, na. 159

Juni

  • I Will Be Valiant,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 162

  • Love One Another,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 136–37

Julai

  • Search, Ponder, and Pray,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 109

  • I Pray in Faith,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 14

Agosti

  • Dare to Do Right,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 158

  • I Feel My Savior’s Love,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 74–75

Septemba

  • Teach Me to Walk in the Light,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,177.

  • Love Is Spoken Here,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 190–91.

Oktoba

  • Seek the Lord Early,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto,108

  • I Lived in Heaven,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 4

Novemba

  • Families Can Be Together Forever,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 188

  • Chagua Jema,” Nyimbo za Dini, na. 135

Desemba

  • We’ll Bring the World His Truth,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 172–73

  • The Hearts of the Children,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 92–93

Kutumia Muziki ili Kufundisha Mafundisho

Muda wa kuimba umekusudiwa kuwasaidia watoto wajifunze kweli za injili. Mawazo yafuatayo yanaweza kukuvutia wakati ukipanga njia za kufundisha kanuni za injili zinazopatikana katika nyimbo za dini na nyimbo za Watoto.

Soma maandiko yanayohusiana. Kwa nyimbo nyingi katika Kitabu cha Nyimbo za Watoto na kitabu cha nyimbo za dini, marejeleo kwenye maandiko yanayohusiana yameorodheshwa. Wasaidie watoto wasome baadhi ya sehemu hizi, na zungumza kuhusu jinsi maandiko yanavyohusiana na wimbo. Ungeweza pia kuorodhesha marejeleo machache ya maandiko ubaoni na waalike watoto walinganishe kila rejeleo na wimbo au mstari kutoka kwenye wimbo.

Jaza nafasi zilizo wazi. Andika ubeti wa wimbo ubaoni kwa kuacha baadhi ya maneno muhimu. Kisha waombe watoto waimbe wimbo huo, na kusikiliza maneno ambayo yatajaza nafasi zilizoachwa wazi. Wakati wakijaza kila nafasi iliyo wazi, jadilini ni kanuni gani za injili mnajifunza kutokana na maneno yanayokosekana.

watoto wakiimba

Toa ushuhuda. Toa ushuhuda mfupi kwa watoto kuhusu kweli za injili zinazopatikana kwenye wimbo wa Watoto. Wasaidie watoto waelewe kwamba kuimba ni njia mojawapo wanayoweza kutoa ushuhuda na kumsikia Roho.

Simama kama shahidi. Waalike watoto wafanye zamu kusimama na kueleza kile wanachojifunza kutoka kwenye wimbo wanaoimba au jinsi wanavyojisikia kuhusu kweli zilizofundishwa katika wimbo huo. Waulize wanajisikiaje wakati wanapoimba wimbo na wasaidie watambue ushawishi wa Roho Mtakatifu.

Tumia picha. Waombe watoto wakusaidie kupata au kutengeneza picha ambazo zinaendana na maneno muhimu au virai katika wimbo. Waalike waeleze ni jinsi gani picha zinahusiana na wimbo na wimbo huo unafundisha nini. Kwa mfano, kama unafundisha wimbo “When He Comes Again” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 82–83), ungeweza kuweka picha kote chumbani ambazo zinaonesha maneno muhimu kutoka kwenye wimbo (kama vile malaika, theluji, na nyota). Waombe watoto wakusanye picha hizo na wazinyanyue juu katika utaratibu sahihi wakati mkiimba wimbo pamoja.

Shiriki somo la vitendo. Unaweza kutumia vitendo ili kuhamasisha mjadala kuhusu wimbo. Kwa mfano, mnapoimba wimbo “My Heavenly Father Loves Me,” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 228–29), ungeweza kuwaonyesha watoto picha ya vitu kama ndege, nyasi, mvua, na maua. Hii ingeweza kuongoza kwenye mjadala kuhusu jinsi tunavyoweza kupata ishara za upendo wa Baba wa Mbinguni kote kutuzunguka sisi.

Alika kushiriki uzoefu binafsi. Wasaidie watoto waunganishe kanuni zilizofundishwa kwenye wimbo na uzoefu ambao wamekuwa nao wa kanuni hizi. Kwa mfano, kabla ya kuimba “I Love to See the Temple” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 95), ungeweza kuwaomba watoto wainue mikono yao kama wamewahi kuona hekalu. Waalike, wanapoimba, wafikirie kuhusu jinsi wanavyojisikia wanapoliona hekalu.

Uliza maswali. Kuna maswali mengi ambayo unaweza kuuliza wakati mnapoimba nyimbo. Kwa mfano, unaweza kuwauliza watoto wanajifunza nini kutoka kwenye kila ubeti wa wimbo. Pia unaweza kuwaomba wafikirie maswali ambayo yanajibiwa na wimbo huo. Hii inaweza kuongoza kwenye majadiliano kuhusu kweli zinazofundishwa katika wimbo.

Tumia matendo rahisi ya mikono. Waalike watoto wafikirie kuhusu matendo rahisi ya mikono ili yawasaidie kukumbuka maneno na jumbe za wimbo. Kwa mfano, mnapoimba “Search, Ponder, and Pray” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 109), unaweza kuwaalika watoto kuonyesha kwenye macho yao wanapoimba kuhusu kupekua maandiko, kuonyesha kwenye vichwa vyao wanapoimba kuhusu kutafakari, na kukunja mikono yao wanapoimba kuhusu kusali.