“Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani:Agano la Kale 2026 (2026)
Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani
Nyenzo Hii Ni Kwa Ajili ya Nani?
Njoo, Unifuate ni kwa ajili ya mtu ye yote anayetaka kujifunza kutoka katika maandiko—kibinafsi, kama familia, na katika madarasa ya Kanisani. Kama hukuwa ukijifunza maandiko mara kwa mara huko nyuma, nyenzo hii inaweza kukusaidia kuanza. Kama tayari una mazoea mazuri ya kujifunza maandiko, nyenzo hii inaweza kukusaidia upate uzoefu mwingi wenye maana.
Watu Binafsi na Familia Nyumbani
Mahali sahihi pa kujifunza injili ni nyumbani. Walimu wako kanisani wanaweza kukusaidia, na unaweza kupata uhamasisho kutoka kwa waumini wengine wa kata. Lakini kunusurika kiroho, wewe na familia yako mnahitaji kulishwa kwa “neno nzuri la Mungu” (Moroni 6:4: ona pia Russell M. Nelson, “Maneno ya Ufunguzi,” Liahona, Nov. 2018, 6–8).
Tumia nyenzo hii katika njia yoyote ambayo ina manufaa kwako. Miuhtasari hii inaonyesha baadhi ya kweli za milele zinazopatikana katika Agano la Kale. Pia inapendekeza mawazo na shughuli ili kukusaidia wewe kujifunza maandiko wewe binafsi, pamoja na familia yako, au pamoja na marafiki. Unapojifunza, fuata mwongozo wa Roho ili kupata kweli za milele ambazo zinaleta maana kwako. Tafuta jumbe za Mungu kwa ajili yako, na kufuata misukumo unayopokea.
Walimu na Wanafunzi Kanisani
Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani ni mtaala kwa ajili ya madarasa ya Jumapili katika Msingi, Shule ya Jumapili kwa vijana na watu wazima,i, madarasa ya Wasichana, na mikutano ya akidi za Ukuhani wa Haruni. Kama unafundisha katika mojawapo ya mazingira haya, unahimizwa kutumia mihutasari katika nyenzo hii kwa ajili ya kujifunza kwako binafsi na unapojiandaa kufundisha. Anza kwa kuwa na uzoefu wako mwenyewe katika maandiko. Maandalizi yako muhimu zaidi yatatokea wakati unapopekua maandiko na kutafuta mwongozo wa Roho Mtakatifu. Tafuta kweli za milele ambazo zinakusaidia uwe zaidi kama Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Njoo, Unifuate inaweza kukusaidia utambue baadhi ya kweli hizi na kuelewa muktadha wa maandiko.
Weka akilini kwamba kujifunza injili, katika ubora wake, ni inapokuwa kitovu chake ni nyumbani na kusaidiwa na Kanisa. Kwa maneno mengine, jukumu lako kubwa ni kuwasaidia watu unao wafundisha katika juhudi zao za kujifunza na kuishi injili nyumbani. Usijali kuhusu kuwa na maudhui ya kipekee ya kuwapa wao darasani. Badala yake, wape fursa ya kushiriki uzoefu wao, mawazo, na maswali kuhusu vifungu vya maandiko walivyosoma nyumbani. Waalike washiriki kweli za milele walizozipata. Hii ni muhimu zaidi kuliko kumaliza kusoma tu kiasi fulani cha nyenzo.
Madarasa ya Shule ya Jumapili ya Vijana na Watu Wazima
Sababu moja muhimu ya sisi kukutana katika madarasa ya Shule ya Jumapili ni kusaidiana na kuhimizana pale tunapojitahidi kumfuata Yesu Kristo. Njia rahisi tunayoweza kufanya hivyo ni kuuliza swali kama vile “Roho Mtakatifu amekufundisha nini wiki hii wakati ulipojifunza maandiko?” Majibu ya swali hili yangeweza kuongoza kwenye majadiliano yenye maana ambayo yanajenga imani katika Yesu Kristo na Injili Yake.
Kisha ungeweza kualika majadiliano yaliyojikita kwenye mapendekezo ya kujifunza katika Njoo, Unifuate. Kwa mfano, wazo la kujifunza linaweza kupendekeza kupekua Isaya 53, ukitafuta maneno ambayo yanaelezea misheni ya Mwokozi. Unaweza kuwaomba washiriki wa darasa kushiriki mawazo au hisia zozote ambazo maneno haya yaliwavutia. Ama mngeweza kutumia sehemu ya muda ukitafuta maneno haya pamoja kama darasa.
Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana
Wakati akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana wanapokutana Jumapili, dhumuni lao ni tofauti kwa kiasi fulani na darasa la Shule ya Jumapili. Kama nyongeza ya kusaidiana kujifunza injili ya Yesu Kristo, makundi haya pia yanakutana ili kushauriana pamoja kuhusu kutimiza kazi ya wokovu na kuinuliwa (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 1.2). Wanafanya hivi kwa maelekezo ya urais wa darasa na akidi.
Kwa sababu hii, kila mkutano wa akidi au darasa linapaswa kuanza na mshiriki wa urais wa akidi au wa darasa akiongoza mazungumzo kuhusu juhudi, kwa mfano, kuishi injili, kuwahudumia watu walio na uhitaji, kushiriki injili, au kushiriki katika kazi ya hekalu na historia ya familia.
Baada ya muda huu wa kushauriana pamoja, mwelekezi anaongoza darasa au akidi katika kujifunza injili pamoja. Viongozi watu wazima au washiriki wa darasa au akidi wanaweza kupangiwa kufundisha. Urais wa darasa au wa akidi, ukishauriana na viongozi watu wazima, hupanga majukumu haya.
Watu waliopangiwa kufundisha wanapaswa kujiandaa kwa kutumia mapendekezo ya kujifunza katika muhtasari wa kila wiki wa Njoo, Unifuate. Katika kila muhtasari, ikoni hii huonyesha shughuli ambayo kwa upekee inahusiana na vijana. Hata hivyo, mapendekezo yoyote katika muhtasari huu yanaweza kutumiwa kama shughuli kwa ajili ya vijana.
Kwa ajili ya mfano wa ajenda za mikutano ya akidi na madarasa, ona kiambatisho D.
Watoto
Maandalizi yako kwa ajili ya kufundisha Msingi huanza kwa kujifunza kwako maandiko wewe binafsi na pamoja na familia yako. Unapofanya hivyo, sikiliza misukumo na umaizi wa kiroho na kutoka kwa Roho Mtakatifu kuhusu watoto katika darasa lako la Msingi. Kuwa mwenye kuomba, na Roho anaweza kukupa mwongozo wa kiungu na mawazo ili uwasaidie wao kujifunza injili ya Yesu Kristo.
Unapojiandaa kufundisha, unaweza kupata mwongozo wa kiungu wa ziada kwa kupekua mawazo ya kufundisha katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Nyumbani na Kanisani. Kila muhtasari katika nyenzo hii una sehemu yenye kichwa cha habari “Mawazo kwa ajili ya Kufundisha Watoto.” Fikiria mawazo haya kama mapendekezo ya kuchochea kupata mwongozo wako wa kiungu. Unawajua watoto katika darasa lako la Msingi—na utapata kuwajua hata vizuri zaidi pale unapo changamana nao darasani. Bwana ana wajua pia, na Yeye atakupa mwongozo wa kiungu wa njia iliyo bora zaidi ya kuwafundisha na kuwabariki.
Inawezekana kwamba watoto katika darasa lako watakuwa tayari wamefanya baadhi ya shughuli hizi katika Njoo, Unifuate pamoja na familia zao. Hiyo ni SAWA. Kurudia rudia ni vyema. Fikiria kuwaalika watoto kushiriki wao kwa wao kile walichojifunza nyumbani—ingawa unapaswa pia kupanga njia za watoto kushiriki hata kama hawakujifunza nyumbani. Watoto hujifunza kweli za injili kwa ufanisi zaidi wakati kweli hizi zinapofundishwa kwa kurudiwa rudiwa kupitia shughuli mbalimbali. Ikiwa unaona kuwa shughuli fulani ya kujifunza inafaa kwa watoto, fikiria kuirudia, hasa ikiwa unawafundisha watoto wadogo zaidi. Unaweza pia kurejelea tena shughuli kutoka kwenye somo lililopita.
Katika miezi ambayo ina Jumapili tano, walimu wa Msingi wanahimizwa kubadilisha muhtasari wa Njoo, Unifuate uliopangwa kwenye Jumapili ya tano kwa shughuli moja au zaidi za kujifunza katika “Kiambatisho B: Kwa ajili ya Msingi—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote Kwenye Njia ya Agano ya Mungu.”