Liahona
Njia ya Agano yenye Shangwe
Liahona Februari 2026


“Njia ya Agano yenye Shangwe,” Liahona, Feb. 2026.

Ujumbe wa kila mwezi wa Liahona Februari 2026.

Njia ya Agano yenye Shangwe

Maajabu na ukuu wa wanafamilia waliounganishwa pamoja katika uwepo wa Baba na Mwana huleta heshima na shangwe tele kwenye nafsi yangu na hunijaza na roho ya shukrani.

Mzee Patrick Kearon na mke wake, Jennifer

Mzee Patrick Kearon na mke wake, Jennifer

Wakati Israel na Elizabeth Haven Barlow walipoondoka Nauvoo, Illinois kwenda Bonde la Salt Lake mwaka 1848, walimwacha nyuma mtoto wa kiume aliyezikwa katika makaburi madogo ya Nauvoo. Mtoto mdogo James Nathaniel Barlow, mtoto wao wa kwanza, alifariki muda mfupi tu baada ya kuzaliwa Mei 1841.

Na kuondoka kwao kwenda Bonde la Salt Lake, Israel na Elizabeth huenda hawakutarajia kutazama tena kaburi la mwana wao. Lakini wakati Israel alipoitwa kwenye misheni ya Uingereza miaka michache baadaye, alipitia Nauvoo alipokuwa akisafiri kuelekea mashariki. Kwa ombi la Elizabeth, alisimama ili kuona lilipo kaburi la mwana wao na kuhamishia mabaki yake kwenye makaburi makuu, mashariki mwa mji.

Baada ya siku nzima ya upekuzi usio na matunda, Israel alitafuta msaada kutoka kwa mtunzaji wa eneo hilo. Siku iliyofuata, walilipata lile kaburi, likiwa karibu na Mary binamu wa James. Kwa kusikitisha, majeneza yalikuwa yameoza na kuvunjika. Katika barua kwa mke wake, Israel aliandika, “Kwa hiyo niligeuka na kuhitimisha kwamba nitawaacha hapo hadi wakati ujao.”

Hakuwa ametembea mbali kutoka kaburini hapo wakati aliposikia sauti. Akikumbuka tukio hilo, aliandika, “Haikuwa yenye kutoa sauti kubwa, lakini iliyosikika kwa urahisi kwenye akili yangu kiasi kwamba sikuweza kuikaidi: ‘Baba, usiniache hapa.’” Israel alirudi kwenye kaburi lile, akihitimisha kumuondoa mvulana wake mdogo baada ya yale yote. “Nilihisi utulivu wa kipekee sana na amani ya akili ambayo sikuihisi hapo awali. … Kiasi hiki nitasema: kwamba kamwe sikuwahi kuwa na umakini zaidi wa wajibu wowote uliofanywa katika maisha yangu kama huu.”

Mnamo Septemba 2, 1853, Israel Barlow na mtunza makaburi yule waliihamisha miili ya James na Mary kwenda kwenye makaburi makuu ya Nauvoo, wakiyawekea alama mahali hapo kwa “mawe kichwani na mguuni mwa makaburi hayo.”

Israel alimwambia Elizabeth kwamba alipokuwa akikaa makaburini hapo, “Nilihisi hamu ya kujitolea mwenyewe kwa dhati na yote ambayo naweza kufanya katika mikono ya Bwana, ili niweze kuhesabiwa kuwa mwenye kustahili kufufuka na [James] asubuhi ya Ufufuko wa Kwanza.”

Kujitolea kwa dhati kwa Israeli kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo, ikiambatana na kuheshimu maagano matakatifu, humruhusu Kristo kufanya uzima wa milele—baraka ile kubwa kuliko zote—iwezekane kwake yeye, mababu zake, na uzao wake.

Ndivyo ilivyo kwetu sisi sote.

trei za sakramenti

Picha na Jerry Garns, inaweza kunakiliwa kwa matumizi ya Kanisa pekee

Ahadi Takatifu

Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, wanampenda kila mmoja wetu kupita kitu chochote tunachoweza kufikiria. Hakuna popote pendo Lao linadhihirika zaidi kuliko kupitia baraka zilizoahidiwa zinazohusiana na maagano yaliyotolewa kwetu kwenye ubatizo na katika nyumba ya Bwana.

“Mojawapo ya dhana muhimu sana ya dini iliyofunuliwa ni ile ya agano takatifu,” Rais Russell M. Nelson (1924–2025) alifundisha. “Katika lugha ya kisheria, agano kwa ujumla linaashiria makubaliano kati ya pande mbili au zaidi. Lakini katika muktadha wa kidini, agano ni la muhimu zaidi. Ni ahadi takatifu kwa Mungu.

Kila ahadi takatifu tunayoifanya na kuishika inatubariki. Baba wa Mbinguni na Mwokozi wetu Yesu Kristo wanataka kutusogeza karibu zaidi na Wao. Wanataka kutusaidia kujifunza na kukua katika imani na uelewa. Wanataka kutujalia nguvu za mbinguni. Wanataka sisi tupate uponyaji na amani katika ulimwengu ambapo baraka kama hizo huonekana kukosekana. Wanataka sisi tupitie shangwe katika maisha haya na katika maisha yajayo. Kutoka kwenye upendo huu mkamilifu, Wao wanatupatia fursa ya kuingia katika muunganiko wa agano na Wao. Tunayo baraka ya kuyaweka upya maagano hayo kila wiki wakati wa mkutano wa sakramenti.

Tunashiriki sakramenti katika roho ya shukrani kwa sababu tunayo baraka ya shangwe ya kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo, tukimkumbuka Yeye na upendo Wake kwetu ulioonyeshwa kupitia zawadi ya Upatanisho Wake—kwamba Aliteseka, alitokwa damu, na kufa kwa ajili yetu. Sakramenti pia hutubariki kwa fursa ya kila wiki ya kuonyesha utayari wetu wa kushika amri Zake, kufanya upya maagano yetu, na kufanya agano jipya (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79).

“Mara nyingi, ninasikia msemo kwamba tunashiriki sakramenti ili kufanya upya maagano tuliyoweka wakati wa ubatizo. Wakati hilo ni kweli, ni zaidi ya hilo,” alisema Rais Nelson. “Nimefanya agano jipya. Ninyi mmefanya agano jipya. … Sasa katika malipo [Bwana] anatoa kauli kwamba daima Roho Wake atakuwa pamoja nasi. Ni baraka iliyoje!”

Tunapotubu na kushiriki sakramenti kwa moyo safi, tunampokea Roho Mtakatifu na “kutakaswa kutokana na dhambi kana kwamba tulibatizwa tena. Hili ni tumaini na rehema ambayo Yesu hutoa kwa kila mmoja wetu.”

Ni shangwe iliyoje kutubu na kusamehewa kupitia upendo wa ukombozi wa Kristo!

Hekalu la Nauvoo Illinois

Picha ya Hekalu la Nauvoo Illinois na Jennifer Rose Maddy

Nyumba Yake ya Shangwe

Baada ya kuwa Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, Rais Nelson alizungumza mara nyingi kuhusu njia ya agano, akianza na ujumbe wake wa kwanza kwa umma kama Rais wa Kanisa. Tunaingia katika njia hiyo kupitia “toba na ubatizo kwa maji“ (2 Nefi 31:17), alisema katika tukio la baadaye, na “kisha tunaingia kwa ukamilifu zaidi ndani ya hekalu.“

Kama vile kushiriki sakramenti kunatukumbusha juu ya maagano yetu na baraka zake husika, vivyo hivyo na kwa kufanya kazi ya uwakilishi hekaluni. Tunapofanya ibada kwa niaba ya wale waliofariki dunia, tunakumbuka ahadi takatifu tulizofanya na baraka zilizoahidiwa tutakazopokea.

Kupitia njia ya agano, tunakuwa warithi wa baraka zote zilizoahidiwa kwa Ibrahimu, Isaka, Yakobo, na uzao wao. Licha ya baraka hizo zilizoahidiwa, Ibrahimu, Isaka na Yakobo hawakuishi maisha rahisi, na hata sisi pia haitakuwa hivyo. Kama wao, tunakabiliwa na dhiki, kurudiwa na upotevu wakati “tunapojaribiwa katika mambo yote” (Mafundisho na Maagano 136:31; ona; pia 101:4–5). Lakini kama manabii na Watakatifu wenye haki wa kale, tunajua ni nani tunaweza kumtumainia (ona 2 Nefi 4:19).

Maisha yetu ya duniani ni muda tu katika kuwepo kwetu, lakini wakati huo—wakati mwingine ni mgumu sana—ni wenye umuhimu wa milele. Ndio, Baba yetu wa Mbinguni anataka tujifunze na kukua. Na, ndiyo, ukuaji huo wakati mwingine unahitaji kukatishwa tamaa na mateso. Lakini Yeye anataka maisha yetu yawe mazuri na yenye matumaini. Kwa hitimisho hilo, na kurahisisha safari yetu ya kurudi Kwake, ametupatia Mwokozi, ambaye ni “mdhamini” wa maagano yetu na Baba Yake. Kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, Baba hutimiza ahadi zilizofanywa kwa watoto Wake hekaluni.

Kupitia upendo Wake na dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Mwokozi wetu ameshughulika na kuponya kila kitu tutakachokabiliana nacho maishani. Na kwa sababu ya nyumba Yake takatifu—nyumba Yake ya shangwe—yote yatakuwa vyema licha ya dhiki. Malhamu (tulizo) ya kushika maagano huondoa huzuni, maumivu, machungu, na kukata tamaa. Hatuhitaji kuwa na hofu au kuogopa. Badala yake, tunaweza kushangilia kwamba thamani ya ukombozi wetu imelipwa (ona 1 Wakorintho 6:20) na kwamba njia ya agano kuelekea uzima wa milele imewekwa.

Njia ya agano hakika ni njia ya upendo wa ukombozi. Tunapoheshimu maagano tunayofanya hekaluni, tunapokea baraka za nguvu kubwa zaidi, upendo mkuu zaidi, rehema kuu zaidi, uelewa mkubwa zaidi, na tumaini kubwa zaidi. Maajabu na ukuu wa kuunganishwa hekaluni—wa wanafamilia waliounganishwa pamoja katika upendo kwa milele yote—huleta heshima na shangwe tele katika nafsi yangu na hunijaza kwa roho ya shukrani.

“Wakati wowote mabadiliko ya aina yoyote yanapotokea katika maisha yako, mahali salama zaidi pa kuwa kiroho ni kuishi ndani ya maagano yako ya hekaluni!” Rais Nelson alishauri. Ninajua ukweli wa maneno hayo kutokana na nyakati za nzuri na chungu za uzoefu wangu mwenyewe wa maisha ya duniani.

kielelezo cha wanandoa wakiwa wamemshika mtoto mchanga

James Nathaniel Barlow, mtoto wa kwanza wa Israel na Elizabeth Barlow, alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa Mei 1841. Miaka mingi baadaye, aliunganishwa na wakala kwa wazazi wake katika Hekalu la Logan Utah.

Kielelezo na Allen Garns

Wakusanye Nyumbani

Baada ya Israel Barlow kusema kwaheri ya mwisho kwa mvulana wake mdogo, alimwandikia mkewe, “Mawazo ya kujiweka kwangu mbali sana, na kamwe katika maisha yangu nisirudi kwenye kaburi la [James], yalikamua uzi wa mwisho wa upendo niliobeba hadi yalipovunjwa kwa machozi kaburini pake.”

Nafikiria kwamba machozi zaidi—machozi ya shangwe wakati huu—yalimwagwa mnamo Desemba 4, 1889. Siku hiyo, mtoto James Nathaniel Barlow aliunganishwa kwa wazazi wake katika Hekalu la Logan Utah. Wakati huo, Israel alikuwa amekwisha fariki dunia, hivyo wengine walisimama kama mawakala kwa ajili yake yeye na Yakobo.

Mimi na Dada Kearon tunayo hisia fulani na huruma kubwa kwa Israel na Elizabeth. Mtoto wetu wa kwanza, mvulana aliyeitwa Sean, alifariki wakati wa upasuaji wa moyo alipokuwa na umri wa wiki tatu tu. Huu ulikuwa ni upotevu mkubwa kwetu. Wakati huo, tulijiuliza kama tungeweza kunusurika. Tulimzika kwa uchungu mkubwa katika kaburi dogo huko Uingereza. Miaka kumi na mitano baadaye, familia yetu iliombwa kuhama kutoka nyumbani kwetu huko Uingereza ili kuhudumu muda wote katika Kanisa, na tuliacha kaburi lile dogo nyuma.

Hatukumpoteza mtoto wetu kwenye msafara wa kwenda magharibi, na hatukuteseka na ugumu usioelezeka wa Barlows, lakini tunao mwanzo wa uelewa wa kile walichopitia. Kaburi la mtoto wetu wa kiume liko mbali sana, lakini kama Barlows, tunayo imani ya kudumu katika Ufufuko wa Yesu Kristo na asili ya milele ya familia yetu kupitia agano takatifu la kuunganisha.

Sisi sote tunao mababu na wapendwa wengine ng’ambo ya pili ya kaburi ambao wanatuambia, “Usiniache hapa.” Kwa sababu ya maagano ya hekaluni, hakuna mtu anayehitaji kuachwa nyuma. Wito wetu ni kuwapenda, kuwahudumia na kusaidia kuwakusanya nyumbani.

Baba yetu wa Mbinguni anatupenda sisi, wewe na mimi. Ametupatia mahekalu ili kwamba “lolote [tukalolifunga] duniani litakuwa limefungwa mbinguni” (Mafundisho na Maagano 128:8; pia Mathayo 18:18). Alimtuma Mwanawe kuvunja kamba za mauti, akitengeneza njia kwa uhusiano usio na mwisho na muunganiko wa familia za milele.

Hiyo ndiyo sababu tunazo ibada. Hiyo ndiyo sababu tunafanya maagano. Hiyo ndiyo sababu tunajenga mahekalu. Hiyo ndiyo sababu tunajitolea wenyewe kwa dhati kwenye kazi na utukufu wa Mungu (ona Musa 1:39). Na hiyo ndiyo sababu tulimwaga machozi ya shangwe, tukijua kwamba muungano wa milele unatungojea sisi na wapendwa wetu katika uwepo wa Baba na Mwana.

Na tupate shangwe na amani tunaposhika maagano yetu na kujiunga na Bwana katika kazi Yake tukufu ya kuokoa.

Muhtasari

  1. Ona Ora H. Barlow, The Israel Barlow Story and Mormon Mores (1968), 306–8; spelling and punctuation modernized; see also Brent A. Barlow, “Daddy, Do Not Leave Me Here,” Ensign, July 2009, 34–36.

  2. Russell M. Nelson, “Maagano,” Liahona,, Nov. 2011, 86.

  3. Ona “Nastaajabu,” Nyimbo za Dini, na. 106.

  4. Russell M. Nelson, katika Dale G. Renlund, “Msimamo Dhabiti kwa Yesu Kristo,” Liahona, Nov. 2019, 25, note 18.

  5. Yesu Kristo Alituomba Tushiriki Sakramenti,” Liahona, Machi 2021, 7.

  6. Ona Russell M. Nelson, “Tunaposonga Mbele Pamoja,” Liahona,, Apr. 2018, 7.

  7. Russell M. Nelson, “Agano Lisilo na Mwisho,” Liahona, Okt. 2022, 6.

  8. Kwa orodha ya baraka hizo zilizoahidiwa, ona Russell M. Nelson, “Maagano,” Liahona, Nov. 2011, 87.

  9. Ona Russell M. Nelson, “Agano Lisilo na Mwisho,” 10.

  10. Ona Russell M. Nelson, “Agano Lisilo na Mwisho,” 7.

  11. Russell M. Nelson, “Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho,” Liahona, Nov. 2021, 96.

  12. Israel Barlow, katika Ora H. Barlow, The Israel Barlow Story, 308; tahajia na vituo vimeboreshwa.

  13. Tarehe ya kuunganishwa imetolewa na Maktaba ya Historia ya Kanisa.