2025
Mpango wa Mungu kwa ajili ya Familia ya Milele
Liahona la Desemba 2025


“Mpango wa Mungu kwa ajili ya Familia ya Milele,” Liahona, Des. 2025.

Ujumbe wa kila mwezi wa Liahona , Desemba 2025

Mpango wa Mungu kwa ajili ya Familia ya Milele

Familia zinazoukubali mpango wa Mungu, wanapenda kama Mwokozi alivyopenda, na kuheshimu maagano yao siku moja watarithi “baraka za uzima wa milele na utimilifu wa shangwe.”

picha ya Hekalu la São Paulo Brazil

Karibu na mwisho wa misioni yangu, nilishangilia wakati nilipopokea endaumenti na kuunganishwa kwa wazazi wangu katika Hekalu la São Paulo Brazili.

Wazazi wangu, Apparecido na Mercedes, walitoka asili tofauti za kidini, lakini uzoefu wao wa maisha uliwatayarisha kuikubali injili ya urejesho.

Baba yangu alilelewa katika familia nzuri lakini sio ya kidini. Hata hivyo, akiwa kijana alivutiwa na dini. Alisoma Biblia, alihudhuria madarasa ya Biblia, na kujifunza maisha ya Yesu Kristo. Kujifunza kwake kulimsababisha kuwa na hamu kubwa katika injili ya Mwokozi na familia, ikimwacha akiwa na hamu ya kumuoa mtu mwenye uelewa kama wake.

Kinyume chake, mama yangu alitoka kwenye familia ya dini sana. Walikumbatia kanuni za injili, walihudhuria ibada za kanisa, na kwa uaminifu waliiishi dini yao. Kukua katika mazingira hayo, mama yangu alikuwa aina ya mtu ambaye kamwe hakukosa mkutano wa kanisa.

Na hivyo, baada ya wazazi wangu kuoana na mimi na kaka zangu watatu kuzaliwa, walifanya kadiri ya uwezo wao kutulea ndani ya nuru ya ufahamu wao wa kanuni za injili. Siku moja shangazi yangu, ambaye alikuwa mshiriki asiyeshiriki kikamilifu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, alimwambia baba yangu, “Una wavulana wanne, mpendwa. Kama kweli unataka kulea familia yenye kiini katika Kristo na kuwa na Mungu katika familia yako, unahitaji kwenda kanisani kwangu.”

Baba yangu alisikia kile alichosema, lakini hakuchukua hatua yoyote hadi siku wamisionari waliokuwa wakitafuta watu wa kuwafundisha katika ujirani wetu, walipogonga mlangoni kwetu, na kuanza kutufundisha. Kwa haraka alitambua kwamba waliwakilisha kanisa ambalo shangazi yangu alikuwa amemhimiza kulichunguza.

Nuru na Ukweli

Mojawapo ya vitu ambavyo mwanzoni viliwavutia wazazi wangu katika injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo ni Kanisa kuweka umuhimu katika familia na mafundisho kwamba “kazi nyingi za Mungu za wokovu na kuinuliwa zinakamilishwa kupitia familia.” Kabla hawajabatizwa, wazazi wangu walivutiwa sana na kile walichokuwa wakijifunza kiasi kwamba waliwaalika majirani kujiunga nao kwa ajili ya masomo ya wamisionari.

picha za wazazi wa Mzee Soares

Mojawapo ya vitu ambavyo mwanzoni viliwavutia wazazi wangu katika injili iliyorejeshwa ya Yesu Kristo ni Kanisa kuweka umuhimu katika familia.

Walipokutana na wamisionari, na kuendelea kujifunza injili baada ya ubatizo wao, wazazi wangu walijifunza njia za “kuwalea watoto [wao] katika nuru na kweli” na jinsi ya “kuweka utaratibu wa nyumba [yao]” kiroho (Mafundisho na Maagano 93:40, 43).

Walijifunza kwamba “familia ni kitovu cha mpango wa Muumba kwa ajili ya hatima ya milele ya watoto Wake” na kwamba “furaha katika maisha ya familia ina uwezekano mkubwa wa kupatikana inapojengwa juu ya mafundisho ya Bwana Yesu Kristo.”

Walijifunza kwamba “ndoa na familia zenye mafanikio zimejengwa na kudumishwa katika misingi ya imani, sala, toba, msamaha, heshima, upendo, huruma, kazi, na shughuli nzuri za burudani.

Walijifunza kwamba familia zinaweza kuwa za milele na kwamba “uhusiano huu huu uliopo miongoni mwetu hapa utakuwepo miongoni mwetu kule, isipokuwa utazidishiwa utukufu wa milele” (Mafundisho na Maagano 130:2).

Na walijifunza kwamba “lengo kuu la kila fundisho, kila shughuli katika Kanisa ni kwamba wazazi na watoto wao wawe na furaha nyumbani, wawe wameunganishwa katika ndoa ya milele, na kuunganishwa na vizazi vyao.”

Kwa ufahamu huo, walitamani kuunganishwa kama familia ya milele.

Jicho Kuelekea Umilele

Baada ya wazazi wangu kubatizwa, waliishi kile walichokuwa wakijifunza, wakihama kutoka ulimwenguni kwenda kwenye ufalme wa injili. Walifanya kazi kuiunganisha familia yetu kwa kuwa na jioni ya nyumbani na kujifunza maandiko kama familia, kwa uaminifu wakihudhuria mikutano ya Kanisa, na kufanya kazi ya historia ya familia. Kwa juhudi hizo kuelekea umoja, walitarajia kuunda familia iliyo na kitovu chake kwenye mpango wa wokovu na jicho kuelekea katika umilele.

Mnamo mwaka 1965, mwaka ambao wazazi wangu walibatizwa, hekalu la karibu zaidi na São Paulo, Brazili, lilikuwa Mesa, Arizona, umbali wa karibu maili 6,000 (kilomita 9,650). Kusafari ilikuwa ghali mno kwa familia yetu, hivyo wazazi wangu walipaswa kusubiri hadi kuwekwa wakfu kwa Hekalu la São Paulo Brazili mwaka 1978 kabla ya wao kuweza kupokea ibada zao za hekaluni na kuunganishwa. Wakati huo, nilikuwa nikihudumu misioni huko Rio de Janeiro.

Takribani miezi miwili kabla sijahitimisha misioni yangu mnamo Februari 1980, rais wangu wa misioni alituruhusu mimi na mmisionari mwenzangu kusafiri usiku mmoja na washiriki wa kigingi kutoka Rio de Janeiro kwenda hekaluni huko São Paulo ili niweze kupata endaumenti na kuunganishwa na wazazi wangu. Kama wazazi wangu, nilikuwa nimesubiri miaka mingi kwa baraka zilizoahidiwa za ibada na maagano ya hekaluni.

Uzoefu huo ulibadilisha ono langu la siku za usoni na kunipa mtazamo wangu wa kwanza wa ukweli wa maneno ya hivi karibuni ya Rais Russell M. Nelson: “Muda hekaluni utakusaidia kufikiria selestia na kupata ono la wewe ni nani hasa, unaweza kuwa nani, na aina ya maisha unayoweza kuwa nayo milele.”

Muda wangu mfupi hekaluni kwenye tukio lile kwa kina ulishawishi huduma yangu iliyosalia ya umisionari. Pamoja na ono hilo jipya, kushuhudia juu ya hekalu na umuhimu wa mpango wa Mungu kwa familia pia ilikuwa na matokeo ya kudumu katika maisha yangu.

Wakati mimi na mke wangu, Rosana, tulipofunga ndoa miaka miwili baada ya misioni yangu, tuliunganishwa hekaluni tukiwa na ono la kuilea familia yetu ya milele. Ili kufanya hivyo, tulifanya kazi pamoja kubuni tamaduni za familia kama zile ambazo wazazi wetu walikuwa wametufundisha, zote zikilenga kwa Mwokozi, mafundisho Yake, na mafundisho ya manabii Wake wa sasa.

Leo watoto wetu wanawalea watoto wao kwa kanuni hizo hizo za injili ya furaha. Kwetu sisi, familia ni kila kitu kwa sababu tunaelewa kiini cha familia katika mpango wa Mungu.

Kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka, nilipata baraka ya kuwaunganisha watoto wangu watatu kwa wenza wao hekaluni. Kuwatazama machoni mwao wakati walipopiga magoti kwenye madhabahu hekaluni ilikuwa ni tukio zuri sana. Niliweza kuona uzao wangu ukibarikiwa kwa kanuni zile zile za injili ambazo wazazi wangu walikuwa wamenifundisha na ambazo Mimi na Rosana tulikuwa tumewafundisha. Niliweza kuona baraka hizo zikiendelea katika vizazi vijavyo. Na nilikumbushwa ni nani anayefanya yote yawezekane.

seti mbalimbali za matukio ya kuzaliwa kwa Yesu juu ya rafu

Ukumbusho wa Krismasi

Familia ni kitovu cha mpango wa Mungu wa furaha, lakini bila Mwokozi Yesu Kristo, mpango huo usingewezekana. Upatanisho Wake na ibada na maagano yanayopatikana katika injili Yake vinawezesha ahadi ya kuinuliwa.

Rais Nelson ametangaza: “Kuinuliwa ni jambo la kifamilia. Ni kupitia ibada okozi za injili ya Yesu Kristo pekee familia zinaweza kuinuliwa. Lengo kuu tunalojitahidi kulifikia ni kwamba tuwe na furaha kama familia—tupokee endaumenti, kuunganishwa, na kujiandaa kwa ajili ya uzima wa milele katika uwepo wa Mungu.”

Ninapotembelea sehemu ambazo sijawahi kuziona hapo awali, ninajaribu kutafuta tukio dogo la Kuzaliwa kwa Kristo ambalo linamkumbusha Rosana na mimi juu ya Mwokozi. Ninatengeneza mkusanyiko mzuri kabisa.

Wakati tukitafakari mandhari hizo za unyenyekevu za Kuzaliwa kwa Yesu, mimi na mke wangu wakati mmoja tulitafakari, “Ni nini ambacho kwa kweli ni muhimu zaidi katika maisha yetu?” Jibu, bila shaka, ni Mwokozi, injili Yake, na familia yetu. Ili kutukumbusha juu ya upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwetu na kwamba ni kupitia Mwokozi kwamba ahadi ya familia za milele inawezekana, kabla ya Krismasi miaka michache iliyopita tuliweka picha hizo za Kuzaliwa kwa Yesu katika rafu mbili kubwa nyumbani kwetu—na kuziacha pasipo kuzitoa baada ya sikukuu za Krismasi. Desturi hiyo inatusaidia kuweka roho ya Krismasi nyumbani kwetu katika mwaka mzima.

Kila siku tunapotazama matukio hayo ya Kuzaliwa, kwa upole yanatukumbusha juu ya jukumu kuu la Mwokozi katika maisha yetu. Zinatukumbusha kwamba duniani iwe amani sasa (ona Luka 2:14) na furaha ya milele katika ulimwengu ujao vinamtegemea Mwokozi na katika kuheshimu maagano tuliyofanya Naye. Na zinatukumbusha “kwamba alikuja duniani, hata Yesu, ili kusulubiwa kwa ajili ya ulimwengu, na kuchukua dhambi za ulimwengu, na kuutakasa ulimwengu, na kuusafisha kutokana na udhalimu wote;

Ili kupitia kwake yeye wote wapate kuokolewa wale ambao Baba aliwaweka katika uwezo wake na kuumbwa naye” (Mafundisho na Maagano 76:41–42).

Kama vile tulivyojifunza kweli hizi kutoka kwa wazazi wetu, Mimi na Rosana tumefanya kazi kuzipasisha kwa watoto wetu. Sasa watoto wetu wanafundisha kweli hizi hizi kwa watoto wao. Mbegu zilizopandwa katika mioyo ya wazazi wangu miaka 60 iliyopita katika nyumba yetu ndogo huko Brazil zimechanua na kuzaa matunda “ambayo ni ya thamani sana, ambayo ni matamu kupita kiasi, na ambayo ni meupe kupita kiasi, ndio, na safi kupita kiasi” (Alma 32:42).

Ninashuhudia kwamba wale wanaoukubali mpango wa Mungu kwa ajili ya familia, wanapenda kama Mwokozi alivyopenda, na kuheshimu maagano yao siku moja watarithi “baraka za uzima wa milele na utimilifu wa shangwe” pamoja na wapendwa wao na Baba na Mwana.