Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana
Baada ya Makosa Yako—Hata Yale Makubwa
Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana Aprili 2026


Ujumbe wa kila mwezi wa Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Aprili 2026

Baada ya Makosa Yako—Hata Yale Makubwa

Tunaweza kujifunza zaidi kutoka kwa Petro kuhusu Mwokozi, Upatanisho Wake, na kujaribu tena.

Petro akimkana Kristo

Kanusho la Petro, na Carl Bloch

Wengi wetu tumetengeneza angalau kumbukumbu moja ambayo tunatamani tungeweza tu kuisahau. Iwe ilikuwa wakati wa aibu halisi, ajali yenye kuleta maumivu ya kimwili, au wakati uliposema maneno unayotamani usingeyasema, kuna nyakati nyingi katika maisha ambapo kitufe cha "rekebisha" au "futa" kinaonekana cha kutamanisha sana.

Unabii wa Kutia Uchungu Ulitimizwa

Mtume Petro alikuwa mtu wa kuvutia katika Agano Jipya. Alikuwa na imani na ujasiri wa kutembea juu ya maji kuelekea kwa Yesu, lakini muda mfupi tu baadaye aliruhusu woga wake kumshinda na kuanza kuzama, akimlilia Bwana kwa ajili ya msaada (ona Mathayo 14:28–31). Wakati hatujui kila kitu katika maisha ya Petro, tunajua wakati mmoja alipolia kwa uchungu.

Saa chache tu kabla ya Yesu Kristo kukamatwa, Yeye alitoa unabii kwamba Petro angemkana mara tatu kabla ya jogoo kuwika mara mbili. Petro alikataa kuamini unabii kama huo na "akanena kwa ukali zaidi, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe." (Marko 14:31).

Bila shaka, unabii wa Mwokozi uligeuka kuwa kweli. Kwa hofu na uwoga vilivyozunguka kukamatwa kwa Mwokozi, ujasiri wa Petro ulimwangusha. Baada ya tayari kukataa mara mbili kwamba hakumjua Mwokozi, na akishinikizwa mara ya tatu, Petro "akaanza kulaani na kuapiza, simjui mtu huyu mnayemnena." (Marko 14:71).

Wakati jogoo alipowika mara mbili na Petro akikumbuka unabii wa Mwokozi, "yeye … akalia kwa majonzi" (Mathayo 26:75).

Lakini huo sio mwisho wa hadithi yake!

Ugeukaji, wa Milele

Kwa yote tunayoweza kujifunza katika maandiko, uwoga wa Petro kamwe haukushinda tena ushuhuda wake juu ya Yesu Kristo. Alishuhudia kwa ujasiri juu ya Mwokozi katika kila fursa, bila kujali hatari ya binafsi katika kufanya hivyo. Kumbuka, Petro alikuwa akiwafundisha watu ambao walikuwa wamemsulubisha Yesu Kristo! Hatari ilikuwa halisi.

Wakati Petro alipomponya mtu kiwete tangu kuzaliwa, akimwamuru, "Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende" (Matendo ya Mitume 3:6), alikamatwa pamoja na Yohana na kuhojiwa jinsi alivyoweza kufanya muujiza huu.

Petro alijibu kwa ujasiri, "Jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.

"Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine wowote: maana hapana jina lingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu, ambalo kwalo lazima tuokolewe" (Matendo ya Mitume 4:10–12).

Ni jibu la ujasiri kiasi gani! Na ushahidi wa wazi wa imani yake.

Watumishi Wasio wakamilifu, Wanaoweza Kikamilifu Kuhudumu

Kila mmoja wetu atatenda dhambi katika maisha haya. Licha ya juhudi zetu bora, tutapungukiwa na matumaini yetu na nia zetu mara kwa mara. Kama Rais Jeffrey R. Holland (1940–2025), Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alivyowahi kufundisha, "Isipokuwa katika suala la Mwanawe wa Pekee mkamilifu, watu wasio wakamilifu ndio ambao Mungu amewahi kufanya kazi nao."

Thamani yako ya kiroho haijaelezewa au kuzuiwa na makosa yako—hata yale makubwa! Kwa sababu alitubu na Kristo alimsamehe, kwa Petro kumkana Kristo hakukumzuia yeye baadaye kushuhudia, kufundisha, na kuongoa kwa nguvu kubwa. Maandiko yamejaa mifano ya wanafunzi wengine ambao walitenda dhambi, wakatubu, na kuendelea kwa imani katika Kristo.

Shetani daima atajaribu kukushawishi kwamba makosa yako yanaongezeka na kwamba kamwe hutaweza kuyashinda. Puuza uwongo wake!

Dada Tamara W. Runia, Mshauri wa Kwanza katika Urais Mkuu wa Wasichana, alifundisha: "Unahitaji kusikia hili, kwa hiyo nitasema maneno haya kwa sauti: Wewe si sauti kichwani mwako au makosa uliyoyafanya. Unaweza kuhitaji kusema hivyo kwa sauti pia. Mwambie Shetani, ’Siyo leo.’ Mweke nyuma yako.

"Hisi mvuto huo, huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu ambayo inakugeuza kuelekea kwa Mwokozi wako, na uangalie neema Yake inaingia katika maisha yako na maisha ya wale unaowapenda. Ninaahidi kwamba dakika tunayoleta moyo uliovunjika kwa ujasiri Kwake, Yeye yupo pale mara moja."

Yesu kristo

Christus Consolator, na Carl Bloch

Siku Zako Angavu Mbeleni

Msimu huu wa Pasaka, unapotafakari kikamilifu zaidi Upatanisho wa Mwokozi, kumbuka kwamba uwezo wa kutubu na kujaribu tena ni mojawapo ya karama kuu unazoweza kupokea. Kwa sababu ya Yesu Kristo, makosa yako mabaya zaidi yanaweza kusamehewa na kisha kuondolewa kama minyororo mizito.

"Mwokozi daima ni mwenye nuru zaidi kuliko giza la aibu," Dada Runia amefundisha.

Kwa sababu ya Yesu Kristo, tumaini linaweza daima kuangaza kwa uangavu mbele unapobakia ukifokasi Kwake.